Leo ni siku ambayo imezoeleka kote duniani kwa waumini wa Dini
ya Kikristo kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo kwa kuhudhuria ibada
na baadaye kuwa na sherehe ambazo kwa kiasi kikubwa huhusisha
wanafamilia.
Makanisa mengi hufurika waumini tofauti na siku
nyingine za ibada na viongozi wa kidini hutumia siku hii kutoa ujumbe
mzito wa kukumbusha umuhimu wa siku hiyo katika maisha yao ya kila siku
kiimani na katika jamii yao kuwa wanatakiwa watende matendo mema wakati
wote na kumheshimu Mungu.
Hata hivyo kwa wengi, mahubiri yote yanayotolewa
siku hii huwa ni ya kawaida na yanaonekana kama yamewekwa tu kukamilisha
taratibu za ibada na maadhimisho ya Krismasi kabla ya kwenda kwenye
sherehe na kesho yake kusahau kama kulikuwa na ujumbe wowote muhimu kwao
wakati huu na baadaye.
Ni kutokana na utamaduni huo taifa letu linazidi
kuwa na ongezeko kubwa la kuporomoka kwa maadili katika kila kada.
Wakati huu, taifa liko kwenye sakata kubwa la uchotaji fedha kwenye
Akaunti ya Tegeta Escrow ambalo lilihusisha watu mbalimbali ambao baadhi
yao ni waumini ambao wamekuwa wakihudhuria ibada hizo za Krismasi kila
mwaka na kukutana na ujumbe unaokumbusha kuwa na maadili mema.
Matukio makubwa yaliyotikisa nchi kama ukiukwaji
mkubwa wa haki za binadamu wakati wa Operesheni Tokomeza, mapigano ya
wakulima na wafugaji, ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya, ujambazi,
wizi, rushwa na ufisadi, yameizonga nchi kiasi kwamba maisha yanazidi
kuliweka taifa katika sintofahamu. Watendaji wa haya yote ni walewale
waumini ambao huingia kwenye nyumba za ibada siku kama za leo na
kukumbushwa umuhimu wa kuwa raia wema.
Viongozi wa kanisa, ambao kwa mujibu wa maandiko
matakatifu, wanatakiwa watangulie mbele na kondoo kuwafuata nyuma, nao
sasa wamekuwa wakiripotiwa kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa, ufisadi
na wengine biashara za dawa za kulevya. Kondoo sasa wamekosa kiongozi
wa kumfuata na matokeo yake kila mtu anafanya analodhani ni sahihi na
hivyo nchi kupoteza mwelekeo.
Mambo haya ni lazima yakomeshwe kwa kila njia
inayowezekana. Pia, moja ya njia hizo hizo ni kuitumia siku hii ya
Krismasi vizuri kwa kuifanya kuwa siku ambayo mahubiri na ujumbe
mwingine unaotolewa leo kuwa ni kukumbusha palipokosewa na kutakiwa
kufanya nini huko mbele.
Viongozi wa kidini na Serikali watakuwa
madhabahuni leo kufanya kazi hiyo ya kukumbusha upendo, amani,
mshikamano; kujali yatima, watu wenye ulemavu, wakongwe na maskini;
kuepuka ufisadi, rushwa, wizi, na uovu mwingine. Wajibu wetu ni kuufanya
ujumbe huo uwe na maana siku zote ili kuipa umuhimu siku hii ya
kuzaliwa Yesu Kristo ambaye Wakristo wanaamini alikuja kuokoa wanadamu
kutoka katika dhambi ambazo ndizo zinaiyumbisha dunia ya leo.
Kwa kuzingatia hayo, Krismasi haitaishia kwenye
sherehe pekee, bali itatusaidia kujenga taifa bora lenye kujali maadili,
wema, amani, mshikamano, haki za binadamu, kuwajibika na hali kadhalika
kuchukia uovu wa aina zote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni