Mtuhumiwa wa wizi baada ya kupewa kichapo na wananchi, hapa ni kabla hajauawa.
Wananchi wenye hasira katika kata ya Tandala wilayani Makete mkoa wa Njombe wameamua kujichukulia sheria mkononi, kwa kumpiga hadi kumuua kinyama mtuhumiwa wa wizi ambaye walimkamata kwa madai kuwa ni mwizi wa mifugo
Tukio hilo limetokea jana majira ya saa 11 jioni ambapo kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo ambao walikataa kutaja majina yao wala kupigwa picha, wamesema mtuhumiwa huyo amekamatwa katika kijiji cha Idege, ambapo kwa madai yao walimkamata na vithibitisho ambavyo ni kamba za kufungia mifugo (ng'ombe na mbuzi)
Wamesema wamechoshwa na vitendo vya wizi katika kata yao na wilaya kwa ujumla na kusema kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa na madai ya kuiba mifugo ya watu ambayo ni ng'ombe na mbuzi, katika maeneo ya Tandala, Ibaga, na huko Idege ambapo ndipo alipokuwa akiishi, hivyo vitendo hivyo vimewachosha
Mwandishi alipouliza kama wanauhakika kuwa mtuhumiwa huyo ndiye mwizi wa mifugo walisema ndiyo, lakini hawakutaka kuithibitisha tuhuma hiyo, na kusema ili iwe fundisho kwa wengine watawaua watuhumiwa wote wa wizi watakaowakamata!
"Dawa itakuwa hii, tumechoka kuibiwa, kila mwizi tutakayemkamata dawa itakuwa hii" walisema wananchi hao kwa jazba
Mtandao huu ulishuhudia wananchi hao wakimpa kipigo cha mbwa mwizi mtuhumiwa huyo kwa mateke, fimbo, na mawe jambo lililompelekea mtuhumiwa huyo kufariki dunia baada ya kuvuja damu nyingi
Mtuhumiwa huyo wakati akiendelea kupigwa kulikuwepo na kamba anazotuhumiwa kuwa ni za kufungia mifugo anayoiiba, nguo, begi na mablanketi pamoja na unga
Baada ya taarifa za mauaji hayo kufikishwa kituo cha polisi Makete, polisi walifika eneo hilo na kuuchukua mwili wa marehemu ambao ulionekana kujeruhiwa zaidi sehemu ya kichwa, na kusema taarifa zaidi zitatolewa