promotion

Ijumaa, 14 Novemba 2014

Wavuvi haramu walipukiwa na baruti Tanga



WAKAZI wawili wa Kata ya Tangasisi tarafa ya Pongwe wilayani Tanga wamejeruhiwa viungo mbalimbali vya mwili kwa kulipukiwa na baruti wakati wakivua kwa kutumia zana za uvuvi haramu kwenye kisiwa cha Karange.
Tukio hilo limetokea juzi majira ya saa nane mchana katika kisiwa hicho, ambako majeruhi hao wakiwa kwenye ngalawa yenye namba za usajili TTA 315 wakati wakijiandaa kutegesha baruti hizo ndipo zilipowalipukia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Freisser Kashai, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja majeruhi hao kuwa ni Hamis Omari ambaye amekatika mkono wa kulia na ameumia jicho la kulia, wakati Adamu Selemani amekatika mikono yote miwili pamoja na kupoteza macho yote mawili.
“Hali ya majeruhi wote wawili ambao wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya Bombo ni mbaya, hii inaonyesha ni kwa kiasi gani uvuvi haramu ulivyo na madhara makubwa kwa jamii pamoja na viumbe wa baharini,” alisema Kamanda Kashai.

Hata hivyo, Kamanda Kashai alitumia fursha hiyo kuwataka wakazi wanaoishi maeneo ya bahari kutoa taarifa ya wavuvi haramu ili kuweza kuwachukulia hatua mapema kabla ya kutokea kwa madhara zaidi.

Hakuna maoni: