promotion

Jumanne, 28 Oktoba 2014

Waziri Simba ahimiza upimaji afya


WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sofia Simba, amewataka watanzania kuwa na tabia ya kupima afya mara kwa mara ili kuepuka magonjwa yanayoweza kutibiwa katika hatua za awali.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa matembezi ya hisani yaliyoandaliwa na Taasisi ya Saratani ya Matiti (TBCF), kwa ajili ya kuchangia matibabu na ujenzi wa kituo cha malezi kwa watu wenye saratani.
Kauli mbiu ya matembezi ya mwaka huu ilikuwa; ‘Saratani ikigundulika mapema na kupata matibabu sahihi hupona’.
Alisema kila mwananchi anapaswa kujichunguza afya yake mara kwa mara, ili anapogundulika kuwa na saratani aweze kupata tiba mapema wakati ugonjwa haujafikia hatua mbaya.
“Matibabu ya saratani ni ghali sana, hivyo ukiwahi na ukatibiwa ikiwa katika hatua ya awali inakuwa nafuu kidogo na wanaume wanakabiliwa na hatari ya kupata kansa ya tezi dume, hivyo nao wawe na kawaida ya kujichunguza,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TBCF, Angela Kuzilwa, alisema asasi hiyo ambayo inaendeshwa na wahanga wa saratani, imekuwa ikiwasaidia watu wanaoishi na kutaabika na saratani ya matiti kwa mahitaji tofauti.
Aliyataja baadhi ya mahitaji ni kama kuwapatia huduma ya ushauri nasaha, kuwasaidia kuishi maisha ya kawaida na yenye faida katika jamii baada ya kugundulika kuwa na saratani.
“TBCF inawaomba watanzania wachangie sh 1,000 kupitia mitandao ya M-pesa 110011, Tigo Pesa 0658 955554 na kiasi utakachotoa kitakuwa na thamani kubwa sana kwa mgonjwa wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi,” alisema.

Hakuna maoni: