promotion

Jumanne, 28 Oktoba 2014

Zitto, TPDC watoana jasho

























MVUTANO mkali umeibuka kati ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC), na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), kuhusu mikataba ya gesi nchini.
Katika mvutano huo, PAC inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ilitaka kuiona mikataba hiyo wakati TPDC ikigoma kufanya hivyo, kwa madai kuwa Kamati hiyo ya Bunge haina mamlaka ya kuiona.
Tukio hilo lilitokea jana wakati kamati hiyo ilipotaka kupokea taarifa ya hesabu za Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), za mwaka wa fedha 2012/13 kwa shirika hilo, lakini ikashindwa kufanya hivyo kutokana na mvutano huo.
Akizungumza kabla ya kuanza kuwasikiliza watendaji wa TPDC, Mwenyekiti wa PAC, Zitto, alisema mwaka mmoja uliopita wakati wakiwa wanapitia hesabu za shirika hilo, waliagiza mambo matatu yafanyiwe kazi.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na TPDC kupeleka mikataba yote ya gesi kwa PAC, kuwasilisha mapitio ya mikataba ya gesi na kuwapa taarifa ya ujenzi wa bomba la gesi.
“Ni kutokana na maelekezo yetu hayo, tunaiomba sasa hiyo mikataba kabla hatujaanza kupitia hesabu zenu, la sivyo mtoke muende mkailete,” aliamuru Zitto.
Kauli hiyo ilimfanya Mwenyekiti wa bodi wa Shirika hilo, Michael Mwanda, kusema kuwa mikataba yote wameiwasilisha kwa Waziri wa Nishati na Madini, kwa kuwa yeye ndiye mwenye mamlaka nayo.
Aliongeza kuwa kama wabunge wanaitaka kwa taratibu za kibunge, watapaswa wapitie kwa Spika, Anne Makinda.
Majibu hayo yalimfanya Zitto amuombe Katibu wa Kamati yake, Erick Maseke, kufafanua juu ya sheria hiyo.
Akitoa ufafanuzi huo, Maseke alisema kuwa sheria inairuhusu kamati na wabunge wote kwa ujumla ambao ni wawakilishi wa wananchi, kupata taarifa zote za Serikali isipokuwa tu zile ambazo zitaonekana kuhatarisha usalama wa nchi.
Pia, alisema wamepewa mamlaka kama Kamati ya Bunge kuwawajibisha watendaji wa Serikali, ambao kwa makusudi watawanyima taarifa au nyaraka zozote za Serikali watakapozihitaji kwa ajili ya kuzifanyia kazi.
Baada ya kibano hicho, ndipo Mwanda alinywea na kusema wao wana nakala ya mikataba hiyo, lakini mikataba halisi ipo kwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo.
Akijibu hoja hiyo, Zitto alisema kuwa kama wangewaambia mapema, wala kusingekuwa na mvutano, kwani shida yao ilikuwa kupata mikataba na majibizano yao yalirefusha mjadala bila sababu.
Zitto, alitoa maagizo mengine kwa watendaji hao kuhakikisha hadi kesho kabla ya saa za kazi kuisha, wahakikishe wanaipeleka mikataba hiyo vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Katika hatua nyingine, PAC imemtaka Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (Narco), Salum Shamte, ajitathmini kama anafaa kuendelea na kazi hiyo kutokana na upungufu uliojitokeza baada ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), kupitia hesabu za kampuni hiyo.
Pia, kamati hiyo imeitaka bodi hiyo itathmini kwa wiki tatu kama kuna haja ya menejimenti ya Narco na menejimenti ya ranchi ya Ruvu kuendelea na kazi walizopangiwa na Serikali.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe, mara baada ya kuihoji bodi na menejimenti ya Narco kuhusu upungufu uliojitokeza kwenye ripoti ya hesabu za fedha kwa mwaka 2011/12 na 2012/13.
Filikunjombe alisema kamati imetoa mapendekezo ya kumtaka mwenyekiti wa bodi pamoja na menejimenti hizo, kujitathmini kwa wiki tatu na kupeleka majibu kuwa zimeshindwa kufanya kazi walizopangiwa hata kusababisha shirika kuwa na hali mbaya zaidi.
Alisema haiwezekani bodi na menejimenti hizo zishindwe kujua namna ng’ombe 376 walivyoibiwa katika ranchi ya Ruvu kwa miezi mitatu, hapo hapo waruhusu mifugo iende malishoni bila ya kuhesabiwa.
Alisema kutokana hali hiyo, wanaitaka serikali kupitia Wizara ya Fedha na Uchumi, isiwapatie fedha Narco katika mwaka wa fedha ujao, kwa kuwa wameshindwa kuzitendea haki fedha za walipa kodi.


Filikunjombe, ameitaka bodi hiyo iangalie kwa wiki tatu kama kuna haja kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Narco Dk. John Mbogoma, kuendelea na kazi hiyo baada ya umri wake kuzidi umri wa utumishi serikalini, kwasababu umri wa kustaafu ni miaka 60 na yeye ana miaka 61.

Hakuna maoni: