Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kamwe hautarudi nyuma katika makubaliano yaliyofikiwa juzi, likiwamo la kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Kauli ya Mbowe ambaye ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa imekuja huku kukiwa na maoni kutoka kwa watu mbalimbali wakiukosoa ushirikiano huo na kwamba hautadumu kutokana na viongozi wengi wa kisiasa nchini kuwa na tabia za kutanguliza masilahi binafsi.
Miongoni mwa mambo yanayotajwa kuwa kikwazo kwa viongozi hao ni suala la ruzuku ambayo hutolewa kwa kuzingatia wingi wa wabunge na idadi ya kura za mgombea urais pamoja na suala la mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi hasa katika maeneo ambayo chama zaidi ya kimoja vina nguvu.
Hata hivyo, jana Mbowe alipuuza dhana hiyo kwa kusema: “Historia ya upinzani nchini imetufundisha mengi na tutakuwa wajinga kama muda wote hatukuweza kujifunza.
“Tunafahamu na tunatambua wapo watu ambao walijitahidi sana kutugawa na kutugombanisha, lakini naomba Watanzania watambue kwamba katika hatua hii hatutakubali kugawanyika tena wala kugombana tena.”
Juzi, vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, NCCR Mageuzi, CUF na NLD vilisaini makubaliano ya kushirikiana ikiwa ni pamoja na kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi zote zijazo tukio lililofanyika kwenye mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.
Akizungumzia suala la ruzuku, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema: “Tuna uzoefu wa miaka 24 sasa katika siasa za vyama vingi na siasa za ushindani, kwa hiyo suala la ruzuku haliwezi kutugombanisha kwa sababu tumeamua kwa dhati kuweka mbele masilahi ya nchi.
“Hilo linawezekana kabisa, tumeonyesha mfano kwa sababu pamoja na umaskini wetu, tulisusia Bunge la Katiba na tukakosa zaidi ya Sh3 bilioni. Hii haimaanishi kwamba watu wetu hawakuwa wakihitaji hizo fedha, lakini ni suala la msimamo tu kuhusu masilahi mapana ya nchi.”
Alisema mambo yote yanayofanyika ndani ya ushirikiano huo yamekuwa yakiratibiwa na timu za wataalamu wakiwamo wanasheria kisha mapendekezo husika kuridhiwa na viongozi wakuu, hivyo hakuna shaka kwamba kila jambo litafuata utaratibu huo.
“Tunao wataalamu wengi wakiwamo wanasheria, kwa hiyo hakuna kitakachoshindikana maana sisi hatuongozwi na matakwa ya ruzuku, tunaongozwa na dhamira safi za kutanguliza masilahi mapana ya nchi,” alisisitiza.
Muungano wa Ukawa dhidi ya CCM, ni matokeo ya misuguano iliyojiri wakati wa mchakato wa Katiba. Hatua ya kwanza ilianza kwa Mbowe kuunda Baraza la Mawaziri Kivuli, likiwashirikisha wabunge kutoka vyama hivyo isipokuwa NLD ambacho hakina mwakilishi bungeni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni