mcharoman blogy fahar yako mtanzania
Moshi Waziri Mkuu wa Zamani, Edward Lowassa jana alidhibitiwa na polisi wakati alipokuwa akienda kwenye msiba wa marehemu Peter Kisumo ambaye alizikwa jana katika Kijiji cha Kighare mkoani Kilimanjaro.
Lowassa na msafara wake akiwa na viongozi wa kisiasa akiwemo Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi James Mbatia, mbunge aliyemaliza muda wake wa Jimbo la Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, ulizuiliwa na polisi baada ya kufika katika Kijiji cha Milolo wilayani Mwanga.
Mara baada ya kufika kijijini hapo, magari ya polisi maarufu kama ‘Defender’ yalikutwa yakiwa yamekatisha Barabara ya Moshi- Same, na polisi wakiwa wamevalia kama vile walikuwa tayari kwa lolote, walisimamisha msafara huo. Kiongozi mmoja wa polisi katika eneo hilo aliwaambia wanasiasa hao kwamba hawakuruhusiwa kwenda msibani kwa staili ya msafara kwa vile hakukuwa na shughuli za kisiasa, hoja hiyo ilizusha malumbano yaliyodumu kwa dakika kadhaa. Lowassa na wenzake walipewa sharti na polisi kwamba waruhusiwe kwenda msibani huku waking’oa bendera zao lakini wafuasi wao warudi walikotoka, jambo ambalo Lowassa alilipinga na kuamua kugeuka na msafara wake kurudi Moshi.
Hata hivyo, walipofika Njia Panda ya Himo, Lowassa alikuta wafuasi wengi ambao walitaka ‘atoe neno’, polisi walikuja juu na kuwazuia kwa madai kwamba watakuwa wanafanya mkutano wa hadhara bila ruhusa au kuomba ulinzi kama sheria inavyotaka.
Baada ya wananchi kukaidi, polisi walifyatua mabomu ya machozi kuwatawanya, hali iliyozusha tafrani katika mji huo mdogo ambao upo njia panda ya kwenda Taveta nchini Kenya.
Wakati hayo yakitokea, katika Kijiji cha Kighare kwenye makaburi ya familia yaliyopo Usangi yalipokuwa yakifanyika mazishi ya mzee Kisumo, hali ilikuwa ya huzuni.
Rais Jakaya Kikwete aliyekuwepo kwenye msiba huo, hakuzungumza chochote na badala yake aliwakilishwa na Waziri wa Sheria na Katiba, Asha Rose Migiro, hata hivyo haikujulikana mara moja kwa nini rais hakuzungumza.
Baadhi ya wafuasi wa Chadema waliposikia Lowassa kazuiliwa kufika, waliondoka kwenye kanisa lililopo Kivindo, katika Tarafa ya Usangi ambako ibada ya mazishi ilifanyika.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, ACP Robert Boaz (pichani) alipoulizwa na gazeti hili kuhusu kuzuiliwa kwa Lowassa na msafara wake alisema kwa wakati huo alikuwa msibani.
“Kwa kuwa sasa nipo msibani siwezi kuzungumzia tukio hilo,” alisema kamanda huyo na kukata simu. Mzee Kisumo aliyekuwa kada mkongwe wa CCM, alifariki dunia Jumanne iliyopita katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni