promotion

Jumamosi, 18 Julai 2015

Ajali, mapigano yaua watu 10

mcharoman blogy fahar yako mtanzania


Watu kumi wamefariki dunia jana katika matukio tofauti ya ajali ya gari na kuteketea kwa moto kwenye matukio yaliyotokea wilayani Siha na Bukoka.
 
Tukio la Bukoba, watu watano wa familia moja wamefariki dunia kwa kuteketezwa na moto na watu wenye hasira kwa madai ya kumuua mfanyabiashara mmoja, wilayani Kyerwa, mkoa wa Kagera. 
 
Aidha, tukio lililotokea wilayani Siha, watu watano wamekufa papo hapo na wengine 11 wakiwa mahututi, baada ya lori la mizigo Mitsubish Fusso, kuigonga Hiace linalofanya safari zake kati ya miji ya Sanya Juu, Wilaya ya Siha na Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro.
 
Ajali hiyo iliyotokea jana saa 12:40 asubuhi katika daraja la mto Kikavu, Wilaya ya Hai, iliyahusisha Fusso lenye namba za usajili T 430 AAQ na Toyota Hiace, T 196 AAW lililokuwa linaendeshwa na dereva anayefahamika kwa jina la ‘Baba D’.
 
Habari zilizopatikana katika eneo la tukio na  kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro (SACP), Fulgence Ngonyani, zinaeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa lori ambaye hata hivyo, alitokomea baada ya kusababisha ajali hiyo.
 
Alisema baadhi ya majeruhi walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na wengine walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi) kwa matibabu. Kamanda Ngonyani alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mawenzi ikisubiri kutambuliwa na ndugu na jamaa zao.
 
Hata hivyo, watu walioshuhudia ajali hiyo, waliieleza NIPASHE  kwamba, dereva wa lori hilo  aliligonga kwa nyuma basi dogo la abiria katikati ya daraja, wakati akitokea katika mji mdogo wa Kwa Sadala na kusababisha vifo hivyo.
 
Grayson Kweka, mkazi wa Kwa Sadala, wilayani hapa alisema, “Huyu dereva wa Fusso alikuwa amepakia mchele na alikuwa akielekea Moshi Mjini, alipofika karibu na daraja la mto Kikavu, lori lilimshinda kutokana na mwendo kasi aliokuwa nao na hivyo kuigonga Hiace na kuua abiria watano papo hapo, akiwamo kondakta wa basi hilo.”
 
Afisa habari na mahusiano wa KCMC, Gabriel Chisseo aliiambia NIPASHE kuwa walipokea majeruhi saba wa ajali hiyo, wakiwa katika hali mbaya na kulazimika kuingizwa katika chumba maalum cha upasuaji.
Aliwataja majeruhi waliolazwa hospitalini hapo kuwa ni Haji Mdangiwa, Fred Urassa, Levina Mnyampanda, Jenista Unonu, Antonia Msaki, Hawa Hamis na Julieth Massawe.
 
Katika tukio la kuteketezwa kwa familia ya watu watano huko Kyerwa, mbali na wananchi hao kuwaua wanafamilia hao, pia wameteketeza mashamba yao yenye ukubwa wa ekari 15 na  nyumba nane na mali  zote zilizokuwemo ndani.
 
Wakizungumza  jana  kwenye  eneo  la  tukio wananchi, walisema  kuwa  watu  wasiojulikana  walipandwa na hasira  baada ya kuwapo kwa  taarifa  za  mfanyabiashara,  Jovinary  Morandi,  kuuawa na kuzikwa kwenye shamba  la  Datusi  Paulo.
 
Walisema watu hao waliwahisi wanafamilia hao kuwa ndiyo wamehusika na mauaji hayo kutokana na Paulo kuwa wakala wa marehemu na pikipiki ya marehemu kukutwa nyumbani kwake.
 
Waliouawa  wametajwa kuwa ni  Datusi  Paulo  (36), Lakius  Paulo (30), Launtina  Henericko (68), Sabiniani Henerico (35) na  mtoto  anayedhaniwa  kuteketea  ndani  ya  nyumba. 
 
Waliobahatika  kutoroka  ni  Adriani  Henerico  na familia  yake ambaye ni  mwalimu katika Shule  ya  Msingi  Mugaba.
 
Akizungumzia tukio hilo, Frolian  Henerico,  mwanafamilia aliyekutwa na kuachwa hai na wananchi hao,  alisema kuwa  wananchi  wa  kijiji  hicho  na  maeneo  jirani walikuwa wamechoshwa  na  vitendo vya  ushirikina na ujambazi walivyokuwa wanafanya wanafamilia  hao.
 
Mwenyekiti  wa  serikali  ya  kijiji  cha  Mugaba, Justinian Clemence, alisema  alifuatwa  nyumbani  na  wananchi  na  ndugu  wa  mfanyabiashara  aliyeuawa  wakiwa  na  mwenyekiti  wa  kitongoji  cha  Omukicherenje wakitaka  kuanza  msako  wa  kumtafuta  ndugu  yao  baada  ya  kutoonekana nyumbani.
 
Clemence alisema kuwa aliwakubalia kwenda kwa mtuhumiwa ambaye alikuwa wakala wa mazao wa mfanyabiashara huyo, na kuwa  baada  ya  kufika    nyumbani  kwa  mtuhumiwa  wakiwa  kwenye  mahojiano  mafupi  waliona  damu  na  kuanza  kufuatilia  ilikoelekea ndipo waliona  sehemu  ikiwa  imechimbuliwa  na  walipofukua  waliona  mwili  wa  mtu  ndipo hasira  za  wananchi zilipoanza.
 
Mkuu  wa  wilaya  ya  Kyerwa,  Luteni  Edward  Ole Lenga, akiongea na wananchi katika eneo la tukio    baada ya kujionea  hali  halisi  aliwataka  kutojichukulia  sheria  mkononi  kwani  kufanya  hivyo  vyombo  vya  usalama  vitakosa  taarifa  muhimu  za  kiuchunguzi.
*Imeandikwa na Godfrey Mushi na Lilian Lugakingira, Bukoba. 

Hakuna maoni: