Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima |
Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema iwapo watu wote watakuwa mstari wa
mbele kudhibiti ajali za barabarani, tatizo hilo litapungua kwa asilimia
kubwa.
Akizungumza bungeni jana wakati akijibu swali la nyongeza la
Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Amina Abdalla Amour, Naibu Waziri wa wizara
hiyo, Pereira Ame Silima, alisema ana uhakika kama wananchi wote
watashiriki kudhibiti ajali tatizo hilo litapungua kwa kiasi kikubwa.
Katika swali lake, Amour alitaka kujua serikali ina mpango gani wa
kuongeza adhabu za makosa ya barabarani hadi kufikia kifungo cha mwaka
ama miaka miwili ili kudhibiti ajali za barabarani ambazo zimekuwa
zikitokea mara kwa mara nchini.
Mbunge huyo alisema ingawa kumekuwa na ufuatiliaji wa kupunguza
ajali za barabarani, lakini bado ajali nyingi zinaendelea kutokea
nchini.
Akizungumzia mikakati ya kupungua ajali, Silima alisema baadhi ya
mikakati ilikuwa ianze kutekelezwa Aprili mwaka huu lakini haikufanikiwa
kutokana na mgomo wa madereva.
Alisema serikali bado inaendelea na majadiliano na madereva ili mikakati hiyo ianze kutekelezwa.
Alisema baadhi ya mikakati hiyo inahitaji fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.
Naye Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM), alisema ongezeko la ajali limekuwa likisababishwa na wembamba na ubora wa barabara.
“Serikali ina mkakati gani wa kuongeza upana wa barabara kwa sababu
ajali nyingi zinatokea kutokana na barabara kuwa nyembamba na
kusababisha magari kugongana uso kwa uso?”alihoji Azzan.
Akijibu, Silima alisema wembamba wa barabara hausababishi ajali za barabarani.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni