Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Mwendokasi jijini Dar es Salaam (Dart), Dk. Asteria Mlambo. |
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Mwendokasi
jijini Dar es Salaam (Dart), Dk. Asteria Mlambo, amewataka waathirika
waliojihifadhi kwenye makalavati ya barabara hizo eneo la Jangwani
kuondoka mara moja.
Pia amewaagiza watendaji wa Dart kuwaelimisha na kuwashauri
waondoke kwa hiyari kwenye maeneo hayo hadi leo jioni kwani si mahali
sahihi pa makazi.
Dk. Mlambo alisema jana kuwa eneo ambalo wakazi hao wamejihifadhi
ni kwa ajili ya matumizi ya barabara na siyo makazi hivyo waondoke.
Alisema, watu hao wanaweza kuiharibu miondombinu kwa kuwa
haikujengwa kwa ajili ya hifadhi ya watu bali kwa atumizi ya barabara,
hivyo shughuli zisizofaa zinazoendelea zitaharibu miundombinu.
“Tayari nimeshawaagiza wafanyakazi wa Dart, waende kuzungumza nao
ili waondoke wenyewe kwa hiyari na ifikapo kesho jioni (leo), asionekane
mtu yeyote kwenye eneo lile la kituo cha mabasi ya mwendokasi,” alisema
Dk. Mlambo.
Alisema wamebaini kuwa wakazi hao ni wale ambao walipewa viwanja
eneo la Mabwepande wilayani Kinondoni, lakini hawakutaka kwenda huko na
pia wengi wao siyo wenye nyumba bali ni wapangaji.
“Wakazi wa mabondeni serikali inawajali, lakini wenyewe hawajijali,
wamepewa maeneo rasmi hawataki kwenda, wamembiwa wahame, lakini
hawataki, sasa sijui wanataka nini,” alisema.
NIPASHE jana lilipita katika eneo la Jangwani na kushuhudia
shughuli za kuzoa taka na michanga katika eneo la daraja zikiendelea.
Katika eneo hilo, Wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi wa Barabara hiyo
Strabag, wakiendelea na shughuli za kusafisha eneo hilo huku mvua
ikiendelea kunyesha.
Rais Jakaya Kikwete, juzi alifika eneo hilo kujionea hali ya
mafuriko na kuwaagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads, kusafisha
eneo hilo la daraja kwa kuzoa taka pamoja na mchanga.
Rais Kikwete alisema taka pamoja na mchanga uliojaa katika eneo
hilo la daraja ndio unasababisha maji kujaa na kusababisha kupita juu ya
daraja badala ya chini ya daraja.
Afisa Habari wa Tanroads, Asha Malima, alisema wameanza kutekeleza agizo la Rais Kikwete.
Malima alisema: “Lile ni agizo la Rais, hivyo sisi tumeshaanza utekelezaji wake na sasa kazi zinaendelea.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni