Mashuhuda wa tukio wameiambia Malunde1 blog kuwa dereva wa lori alikuwa anaendesha gari akiwa katikati ya barabara huku dereva wa basi akiwa katika mwendo kasi hali ambapo katika kukwepa basi hilo aligonga tela la lori kisha kupinduka.
Mmoja wa walionusurika kifo katika ajali hiyo Kelvin Moshi mkazi wa Tanga aliyekuwa anasafiri kutoka Mwanza kwenda Tabora alisema dereva wa basi alikuwa katika mwendo kasi hali ambayo ilimfanya basi limshinde na kugongana na lori hilo.
“Dereva wetu alikuwa katika mwendo kasi,akalikwepa basi na kugonga tela la lori lililokuwa linapandisha mlima katika barabara na kupinduka mara kadhaa,ajali hii imetokana na uzembe wa dereva wetu”,alieleza Moshi.
Diwani wa kata ya Samuye Amos Shija alisema dereva wa basi alikuwa katika mwendo kasi basi likamshinda kisha kugongana na basi hilo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha aliyekuwa eneo la tukio alisema watu 10 wamepoteza maisha katika ajali hiyo kati yao 9 walifariki dunia papo hapo huku majeruhi 50.
“Watu 10 wamefariki dunia,miili mitatu ya marehemu ilinasa kwenye gari,majeruhi waliopo ni 50 wakiwemo wanawake 13,wanaume 36 na mtoto mmoja wa kiume wanapata matibabu katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga,wapo walio katika hali mbaya akiwemo dereva wa basi,tunashukuru wananchi wametusaidia kusaidia majeruhi na kuondoa miili ya watu walionasa kwenye basi”,alieleza Kamanda Kamugisha.
“Basi lilikuwa linatoka Mwanza kwenda Tabora,chanzo ni uzembe wa dereva na mwendo kasi wa basi wakati huo huo dereva wa lori alikuwa anaendesha gari akiwa katikati ya barabara,ndipo yakagongana na kusababisha vifo na majeruhi”,alieleza Kamanda Kamugisha.
Kamanda Kamugisha alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga huku majeruhi wakiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
Alisema tayari dereva wa lori anashikiliwa na jeshi la polisi huku akiwataka madereva kuzingatia sheria za baarabarani ili kuepuka ajali zisizokuwa za lazima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni