promotion

Alhamisi, 19 Machi 2015

Kikwete: Anzisheni maktaba za kumbukumbu za marais.

mcharoman blogy fahar yako mtanzania
 
Rais Jakaya Kikwete (pichani), ameitaka Wizara ya Utumishi ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi la  wa Umma kupitia Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu na Nyaraka, kufikiria uanzishwaji wa maktaba za marais ambazo zitakuwa zinahifadhi kumbukumbu zao.
 
Rais Kikwete aliyasema hayo wakati akifungua rasmi Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu na Nyaraka mjini hapa jana kilichojengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 7.9.
 
Alisema utunzaji wa kumbukumbu za marais waliomaliza vipindi vyao yakiwamo maandishi yao, ziara zao na mawasiliano na viongozi wengine duniani, utasaidia kuhifadhi historia ya marais hao.
 
“Msipohifadhi historia ya marais wenu, mtakuwa mmepoteza kumbukumbu kubwa ya taifa lenu,” alisema na kutoa mfano wa maktaba kama hizo nchini Marekani ambazo zinahifadhi kumbukumbu za magazeti yote duniani likiwamo gazeti la Ngurumo la Tanzania.
 
Alisema Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu ambacho kimejengwa kwa lengo la kuhifadhi kumbukumbu zake kwa dijitali, kina uwezo wa kuhifadhi mafaili zaidi ya 750,000, hivyo kitumiwe kuanzisha maktaba hizo.
 
Alisema Tanzania Bara imebahatika kupata marais katika vipindi vinne hivyo kama zingewekwa kumbukumbu kuanzia za rais wa awamu ya kwanza, itakuwa imehifadhi historia nzuri kwa vizazi vijavyo kwa kuwa watakuwa wanajuwa kila rais alikuwa na fikra gani katika uongozi wake.
 
Akizungumzia kituo hicho, Rais Kikwete alisema kitasaidia kuhifadhi kumbukumbu na kupunguza tatizo la ucheleweshaji wa malipo ya pensheni kwa sababu ya kukosa kumbukumbu nzuri na pia kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi na upotevu wa mali ya umma kwa kuwa kumbukumbu zote zitakuwa zinahifadhiwa kidijitali.
 
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma, Celina Kombani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora, George Mkuchika, alisema kituo hicho kitaisaida kukomesha ugawaji holela wa viwanja na ucheleweshaji wa kesi mahakamani.
 
Mwakilishi wa Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza  (DFID) nchini, Rose Cooper, aliipongeza serikali kwa kujenga kituo hicho ambacho kitaboresha utunzaji wa kumbukumbu.