Siku 10 tu baada ya marehemu Benadetha Steven(35) aliyefariki kutokana na uvimbe tumboni aliyekuwa mkazi wa Mtaa wa Mapinduzi kata ya Ndala katika manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga kuzikwa na kifaranga cha kuku tumboni kwa madai kuwa ndugu wanaondoa mikosi katika familia,kaburi lake limekutwa limefukuliwa na watu wasiojulikana,malunde1 blog inakupa mkasa mzima.
Kaburi la marehemu Benadetha limekutwa limefukuliwa huku sanda na jeneza likiwa linaonekana na alama za nyayo za miguu ya watu na miguu ya mnyama aina ya fisi zikionekana katika kaburi hilo.
Walioshuhudia tukio hilo walisema taarifa za kuwepo kwa tukio hilo la kushangaza zilienea Siku ya Jumatatu Januari 12,2015 jioni na kesho yake Jumanne Januari 13,2015 asubuhi uongozi wa eneo husika ulifika katika makaburi ya kata ya Masekelo katika manispaa ya Shinyanga alikozikwa marehemu huyo na kukuta halisi jinsi kaburi lilivyokuwa limefukuliwa.
Mmoja wa mashuhuda hao Makaranga Mabula(60) alisema tukio hilo linatokana na imani za kishirikina na kwamba tukio la kufukua kaburi ni kwanza kutokea katika kata ya Ndala hivyo kuviomba vyombo vya dola kufanya uchunguzi ili kuwabaini wahusika wa tukio hilo la kinyama.
Mjumbe wa serikali ya mtaa wa Masekelo kata ya Masekelo alikozikwa marehemu Josephine Kishiwa (Chadema)alisema alipokea taarifa za kuwepo kwa tukio hilo siku ya Jumatatu saa moja usiku na kesho yake asubuhi alikwenda kwenye kaburi hilo akiwa na wanamtaa wengine na kukuta kweli kaburi hilo limefukuliwa.
“Tunalaani kitendo hiki,tumekuta jeneza na sanda ya marehemu inaonekana,tukaita polisi,hiki kitendo kimefanywa na binadamu tu maana kaburi lilikuwa refu sana,fisi hawezi kufukua,hapa kuna miguu ya watu na fisi,fisi nadhani alisikia harufu ya maiti,na fisi hawezi kuingia kwenye shimo,binadamu wamekosa utu”,alisema Kishiwa aliopozungumza na Malunde1 blog.
Naye mjumbe wa serikali ya mtaa wa Mapinduzi kata ya Ndala(Chadema) Deogratius Masanja alisema kwa mujibu wa taarifa alizozipata kutoka mume wa marehemu Maulid Omari Njunju ambaye hakutaka kuzungumza na waandishi wa habari,alidai kuwa siku tatu zilizopita ndugu wawili wa marehemu walionekana katika mtaa huo katika mazingira ya kutatanisha.
“Huenda ndugu wa marehemu wamehusika,kwani mume anasema ndugu walionekana hivi karibuni kuja kumalizia kufanya mambo yao ya kimila wakati wa mazishi Januari 3,2015,kaburi limefukuliwa liko juu,huenda hata mwili wa marehemu umechukuliwa”,Masanja aliiambia Malunde1 blog.
Hata hivyo kuna taarifa kuwa juzi nyakati wakati wa usiku watu wasiojulikana wakiwa na gari walionekana eneo la makaburi hivyo kuleta sintofahamu kama ni ndugu wa marehemu ama watu wengine wamehusika katika tukio hilo.
Kufuatia taarifa hizo saa 6 mchana Januari 13,2015 jeshi la polisi lilifika katika kaburi la marehemu na kuuomba uongozi wa eneo husika kuruhusu kaburi la marehemu lifukiwe kwani jeshi la polisi halina na mamlaka ya kufukua mwili bali mahakama ndiyo yenye mamlaka hayo.
Akizungumza katika eneo la tukio mkuu wa upelelezi mkoa wa Shinyanga Musa Athuman Taibu alisema wanalaani tukio hilo linalohusishwa na imani za kishirikina na kukosa hofu ya mungu huku akiwataka wananchi kumrudia mungu na kuwafichua watu wote wanaofanya uhalifu.
“Hili kaburi halijatitia,hii ni tabia mbaya sana,hatuwezi kuvumiliana kwa hali hii,unatafuta nini kwenye kaburi la marehemu,unachukua nini kwa ajili ya nini,nawashauri wananchi kuwa walinzi wa kila mmoja,toeni taarifa za mnayehisi kafanya jambo hili kwa viongozi wenu sisi tutajua cha kumfanya”,alisema Taibu.
Mkuu huyo wa upelelezi mkoa wa Shinyanga alisema jeshi la polisi halina mamlaka ya kufukua kaburi la marehemu bali mahakama pekee ndiyo yenye yenye mamlaka ya kutoa kibali cha kaburi kufukuliwa hivyo kuwaomba wananchi kufukia kaburi hilo badala ya kulifukua.
“Naomba mrudishie udongo,sababu ya kufukua kaburi hatuna,tunatafuta nini kwa marehemu,tunachoamini ndugu yetu alikufa kifo cha kawaida,na alizikwa kawaida,haya mambo yaliyojitokeza ya mila siyo sahihi,ni mila potofu na hazifai kwa jamii,ndiyo maana tunasema ni bora watu wamwamini mungu ili waachane na mila hizi za kishirikina”,aliongeza Taibu.
Kitendo cha kaburi la marehemu kufukiwa bila kufukuliwa kimezua maswali kwa wakazi wa eneo hilo huku wengine wakisema kuwa ni bora kaburi lingefukuliwa kwa hivi sasa hawaamini kama mwili wa marehemu upo kaburini au la kutokana na sanda na jeneza kuonekana juu sana tena kama limetobolewa na udongo kwenye kaburi hilo kuonekana kupungua ukilinganisha na ulivyokuwa siku ya mazishi.
Kitendo cha kaburi la marehemu kufukiwa bila kufukuliwa kimezua maswali kwa wakazi wa eneo hilo huku wengine wakisema kuwa ni bora kaburi lingefukuliwa kwa hivi sasa hawaamini kama mwili wa marehemu upo kaburini au la kutokana na sanda na jeneza kuonekana juu sana tena kama limetobolewa na udongo kwenye kaburi hilo kuonekana kupungua ukilinganisha na ulivyokuwa siku ya mazishi.
Benadetha Steven(35) alikuwa anaishi mtaa wa Mapinduzi kata ya Ndala,alifariki dunia Januari 1,2015,wakati akitibiwa uvimbe wa tumboni katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga na kuzikwa katika makaburi ya Masekelo ambapo mazishi yake yalileta utata baada ya ndugu wa marehemu kutoka mkoani Mara(Wakurya) kuingia kaburini na kuchana tumbo la marehemu kwa wembe kisha kuchinja kifaranga cha kuku kwa wembe na kuingiza kuku huyo kwenye tumbo la marehemu.
Kitendo hicho ambacho ndugu wa marehemu walidai wanaondoa mikosi kwenye familia baada ya kudai wanafamilia wengine kufa kwa ugonjwa wa namna hiyo,waombolezaji waliondoka makaburini wakidai kuwa kitendo cha marehemu kupasuliwa tumbo tena kwa wembe hadharani ni cha fedheha.
Hata hivyo ndugu wa marehemu hawakujali waliendelea kuzika na baadaye kukamatwa na polisi kwa muda na kuhojiwa kisha kuruhusiwa kuzika ndugu yao huku waombolezaji wachache wakijitokeza kujumuika na ndugu wa marehemu kumzika marehemu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni