Wachuuzi wa ndizi katika Soko la Makorora Tanga wakisubiri wateja ambapo walikuwa wakiuza mkungu mmoja kati ya Sh7000 na Sh13000 inategemea na aina ya ndizi na ukumbwa wa mkungu. Picha na Salim Mohammed
Imeelezwa kuwa wakulima wa mahindi mkoani Ruvuma wanaidai Serikali zaidi ya Sh22 bilioni, hali inayowafanya waishi maisha magumu.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alieleza hayo jana katika kikao kati ya wafanyabiashara na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda kilichofanyika mjini hapa.
Alisema asilimia 50 ya mazao hayo yaliyouzwa katika Kitengo cha Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA), hayajalipwa.
“Waziri hadi sasa tunadaiwa na wakulima fedha za mahindi ambayo wametukopesha kwenye kitengo chetu, lakini tunaendelea kuwasiliana na Wizara ya Fedha ili ilipe deni lote.
“Mkulima kuikopesha Serikali ni jambo jema kuliko kumkopesha mtu binafsi ambaye anaweza kukudhulumu, kisha ukashindwa kumdai,” alisema Mwambungu.
Katibu wa wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma, Wilson Nziku alimuomba Waziri Kigoda kuwasaidia wakulima hao walipwe fedha zao mapema ili kuepuka adha katika msimu ujao wa kilimo, ikiwamo kununua pembejeo mapema.
Alisema wakulima wengi wanategemea fedha hizo kuendesha shughuli zao.
Kwa upande wa wakulima hao, waliiomba Serikali kuwalipa madeni yao ili walipe ada za shule kwa watoto wao pamoja na kununua pembejeo.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni