TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Rais mpya wa Mozambique, Mheshimiwa
Filipe Jacinto Nyusi salamu za rambirambi kuomboleza vifo vya watu 79
waliopoteza maisha yao kutokana na kunywa pombe yenye sumu.
Aidha,
Rais Kikwete amewatakia watu wengine 174 ambao wamepata madhara ya viwango
mbali mbali katika tukio hilo, baadhi yao bado wamelazwa hospitali, kupata
nafuu ya haraka, ili waweze kurejea katika shughuli za maendeleo ya nchi yao na
ya maisha yao.
Watu
hao walipoteza maisha yao na wengine kuathirika afya zao wiki iliyopita wakati
walipokunywa pombe inayodhaniwa ilitiwa sumu ya nyongo ya Mamba katika kijiji
cha Chitima, Wilaya ya Cahora Basa, Jimbo la Tete.
Serikali
ya Mozambique imetangaza siku tatu za maombolezo ya taifa na kuamuru bendera zote
kupepea nusu mlingoti. Siku hizo zinamalizika kesho, Alhamisi, Januari 15,
2015.
Amesema
Rais Kikwete katika salamu zake: “Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa
za vifo vya watu 79 ambao wamepoteza maisha yao kwa kunywa pombe yenye sumu
katika Jimbo la Tete nchini mwako. Nakutumia Mheshimiwa Rais salamu zangu za
rambirambi na naungana nawe kuomboleza
vifo vya ndugu zetu hawa.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Nakuomba pia unifikishie salamu
zangu kwa ndugu na jamaa wote ambao wamepoteza wapendwa wao katika tukio hili.
Aidha, kupitia kwako, nawatakia wote ambao wameathirika katika ajali hiyo
kupata ahueni ya haraka na kurudia maisha yao ya kawaida.”
Rais
Kikwete vile vile ametoa pole nyingi kwa Rais Nyusi na Serikali yake kutokana
na madhara ambayo yanasababishwa na mvua kubwa zinazonyesha nchini Mozambique
ambazo pamoja na mambo mengine zilizoa madaraja makubwa matatu na kukata
mawasiliano kati ya eneo la Kaskazini na la Kusini mwa Mozambique.
Imetolewa
na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es
Salaam.
15
Januari,2015
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni