mcharoman blogy
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, amejiuzulu.Jaji Werema amelazimika
kujiuzulu kufuatia shinikizo kubwa kutoka kwa makundi kadhaa ya jamii na
ushauri wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Rais Jakaya Kikwete,
kutaka amfute kazi kutokana na kuhusishwa kwake na kashfa ya wizi wa zaidi ya
Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania
(BoT).
Jaji Werema alijiuzulu jana kupitia barua yake aliyomwandikia Rais Kikwete,
akiomba kujiuzulu kutokana na kashfa hiyo.Taarifa iliyotolewa jana usiku na
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilisema:
“Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, amejiuzulu nafasi yake
hiyo kuanzia leo (jana) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete, amekubali ombi hilo la kujiuzulu.”
Taarifa hiyo ilieleza kuwa katika barua yake kwa Rais Kikwete, Jaji Werema
alisema kuwa ameomba kujiuzulu kwa sababu ushauri wake kuhusiana na suala ya
Akaunti ya Tegeta Escrow hakueleweka na umechafua hali ya hewa.
“Mheshimiwa Rais Kikwete amemshukuru Jaji Werema kwa utumishi wake ulioongozwa
na uaminifu na uadilifu,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo fupi.Sakata la wizi
wa fedha hizo liliibuliwa na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi, David
Kafulila, katika mkutano wa Bunge la Bajeti mwaka huu, lakini serikali
ilikanusha kuchotwa kwa fedha hizo kwa maelezo kuwa hazikuwa za umma.
Miongoni mwa viongozi waandamizi wa serikali waliotoa kauli za kupuuza hoja ya
Kafulila ni Jaji Werema na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Jaji Werema alivutana na Kafulila kuhusiana na sakata hilo na kutoleana maneno
makali, huku Jaji Werema akitishia kumpiga Kafulila, na ugomvi huo
ulisuluhishwa na baadhi ya wabunge na mawaziri ndani ya Bungeni.
Kabla ya kutaka kumpiga, Jaji Werema alimuita Kafulila kuwa ni tumbili na
Kafulila alijibu mapigo hayo kwa kumuita Jaji Werma kuwa ni mwizi.
Kutokana na shinikizo hilo, Waziri Mkuu alimwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi katika akaunti hiyo na kuwasilisha
taarifa hiyo bungeni.
Aidha, Waziri Mkuu aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) kuchunguza tuhuma hizo.
Katika mikutano ya Bunge ya 16 na 17 iliyomalizika Novemba 29, mwaka huu,
wabunge walishinikiza serikali kuhakikisha kwamba ripoti ya CAG inawasilishwa
bungeni na kujadiliwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni