Suala la hali mbaya inayoikabili Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) limefika bungeni, baada ya Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje, kuibana serikali, akiitaka itoe tamko la dharura kunusuru hali hiyo katika hospitali hiyo.
Wenje alifikia hatua hiyo kupitia mwongozo wa Spika aliouomba kwa Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, bungeni jana.
Alisema habari iliyoongoza ukurasa wa kwanza katika gazeti la NIPASHE toleo la jana, ilieleza namna hali mbaya ya huduma iliyopo katika hospitali hiyo.
“Hakuna dawa, hali ni mbaya sana, hospitali ni chafu, vyoo vimeziba, watu wamelala mpaka kwenye korido, hakuna vitanda, hali ni mbaya sana,” alisema Wenje.
Aliomba mwongozo wa spika akitaka kujua kama habari hiyo iliyoandikwa gazeti la NIPASHE ni kweli.
“Na kama ni kweli, serikali inatoa tamko gani la dharura ya kunusuru hali kwenye Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili pamoja na kwamba hospitali zote nchi hii hali ni ovyo ovyo tu kama ilivyo leo kwenye Hospitali ya Muhimbili?" alihoji Wenje.
Aliongeza: “Kwa hiyo, mheshimiwa kupitia kiti chako, naomba kupata tamko la serikali namna gani watanusuru kwa dharura Hospitali ya Muhimbili.”
Akijibu, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alisema inategemea taarifa zinavyotolewa na mtu anavyozitoa.
Hata hivyo, alisema kesho wizara yake itatoa taarifa bungeni kuelezea hali ya Bohari ya Dawa (MSD) pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa nchini, ambayo itatoa picha ya hali ilivyo nchini.
Pia aliwasihi waandishi wa habari kushirikiana na wizara husika katika kutoa taarifa na kuwa hilo litasaidia kuzuia kutoa taarifa, ambazo siyo sahihi, zinazohofisha na kusababisha madhara kwa watu wanaozisikiliza au kuzisoma.
“Sasa kwenye eneo kama hili mimi nilikuwa napenda sana kwamba taarifa zinazotoka kwenye vyombo vya habari basi ni vyema ziwe zimetolewa au kushirikisha wizara husika ili kuhakikisha usahihi wa taarifa kama inavyotolewa.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni