promotion

Alhamisi, 13 Novemba 2014

Apec kuzindua baraza la waendesha bodaboda




SHIRIKA la Kupunguza Umaskini na Kutunza Mazingira nchini (APEC), linajiandaa kuzindua Baraza la Taifa la Waendesha Bodaboda nchini Desemba 15 mwaka huu.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa APEC, Respicius Timanywa, alisema wameamua kuanzisha baraza ili wamiliki na waendesha bodaboda wapate chombo cha kuwaunganisha.
Timanywa, alisema maandalizi ya uzinduzi wa baraza hilo yanaendelea na kwamba, wamepanga uzinduzi huo kufanyika mkoani Singida ambako shirika hilo linaendelea na mafunzo kwa wamiliki na waendesha bodaboda katika kata na vitongoji.
Alisema kuanzishwa kwa baraza hilo, kutawasaidia wamiliki na waendesha bodaboda wote nchini kuamua jambo moja kwa ajili ya kuieleza serikali ama kuwaunganisha pamoja.
Aidha, alisema baraza hilo litaunda kamati mbalimbali za kufuatilia masuala ya shughuli zao za uendeshaji wa bodaboda, nidhamu za kazi hiyo, ulinzi na usalama pamoja na maadili.


Shirika hilo la APEC ambalo lilianzishwa mwaka 2008 na kujikita zaidi katika mafunzo ya wamiliki na waendesha bodaboda, limeshafanya mafunzo katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Mbeya, Njombe, Manyara, Arusha na sasa Singida.

Hakuna maoni: