Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye anaendelea na matitabu yake nchini Marekani, jana, Jumatano, Novemba 12, 2014, anatarajiwa kutoka wodini katika Hospitali ya Johns Hopkins na kuhamishiwa kwenye Hoteli Maalum ambako ataendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari.
Rais Kikwete amekuwa kwenye Hospitali ya Johns Hopkins tokea Jumamosi iliyopita wakati alipofanyikwa upasuaji wa tezi dume (prostrate) na afya yake imekuwa inaimarika kiasi cha kuanza mazoezi ya kutembea.
Kutokana na kuondolewa kwa bandeji kwenye mshono ambao nao umeanza kukauka vizuri, Rais Kikwete baadaye leo atahamishwa kutoka wodini kwenda kwenye Hospitali Maalum yenye uhusiano na Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko karibu na hospitali hiyo.
Akiwa kwenye Hoteli Maalum hiyo, Rais Kikwete ataendelea kupatiwa matibabu, kutembelewa mara kwa mara na madaktari na kuwa chini ya uangalizi wa wauguzi muda wote. Wiki moja baadaye, Rais Kikwete atafanyiwa tathmini ya kuwawezesha madaktari kuamua hatua inayofuata ya matibabu yake.
Wakati huo huo, kwa sababu ya wingi wa ujumbe mfupi wa simu (sms) ambazo amekuwa anazipokea Rais Kikwete, imeanzishwa namba maalum ya simu ambako wananchi wanaweza kuwasiliana kwa sms na Mhe. Rais. Namba hiyo ni +1-646-309-2295.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
12 Novemba, 2014
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni