CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeifananisha hali inayolikumba taifa kwa sasa ambako kila kukicha kumekuwa kukiibuliwa kashfa za ufisadi, ni sawa na kupita kwenye bonde la mauti.
Kutokana na hali hiyo, kimewataka wananchi kuinusuru nchi kwa kufanya mabadiliko ya haraka, kuanzia uchaguzi ujao wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
Akizungumza na wananchi katika vijiji mbalimbali vya Wilaya za Uyui na Urambo mkoani hapa juzi, Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Freeman Mbowe, alisema kuwa kashfa ya sh trilioni 1 ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, ambayo imefichuka wakati kashfa ya IPTL kwenye akaunti ya ESCROW ikiwa haijapata majibu, haitaiacha salama serikali ya CCM.
Mbowe, ameibua tuhuma hizo akisema kuwa baadhi ya viongozi serikalini kwa kushirikiana na viongozi wa CCM, waliongeza gharama ya ujenzi wa bomba kutoka dola mil. 600 za Marekani hadi dola mil. 1,200, ambako kiasi chote kilichoongezwa kwa hila kimeishia mifukoni mwa watu wachache.
Mbowe, ambaye leo anaingia mkoani Katavi kuendelea na ziara iliyoanza Novemba 6, akiwa Uyui, alisema kuwa serikali ya CCM haina nia ya kukomesha ufisadi, ndio maana pesa zinazodaiwa kuchukuliwa kwenye bomba la gesi zimewanufaisha wachache. Akifafanua madai hayo ya ufisadi wa sh trilioni 1, Mbowe alisema kuwa wakati baadhi ya viongozi hao wanafikiria kunenepesha mifuko yao kwa njia batili, wananchi wanakufa na wengine kutaabika kwa kukosa matibabu hospitalini kwa Serikali kushindwa kulipa deni la sh bilioni 90 inalodaiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Aliongeza kuwa, wakati baadhi ya viongozi wanaweka mbele maslahi yao na familia zao, wakitumia vibaya fedha za walipa kodi Watanzania maskini katika ‘kulipia’ ufisadi huo, wananchi wananyanyaswa na kulazimishwa kuchangia michango mbalimbali ikiwemo ujenzi wa maabara.
“Ndugu zangu Watanzania wenzangu, pamoja na kuzungumzia masuala yenu ya tumbaku, mpunga, mbao, manyanyaso ya viongozi wa CCM na serikali yao, naomba pia nizungumze masuala ya kitaifa, ambayo pamoja na kwamba yanafanyika mbali na ninyi hamjui, athari zake zinatugharimu sote kabisa,” alisema.
Aliongeza kuwa; “Kila ufisadi unaofanywa na viongozi wa CCM na serikali yake unatuathiri wananchi, leo hii gharama za ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam…lile ambalo mlisikia wananchi waliandamana, wakapigwa risasi na kutawaliwa kijeshi, zimeongezwa mara dufu ili kutoa ulaji kwa wakubwa…
“Safari hii tuhuma hizi ni kubwa mno, ufisadi huu umevunja rekodi. Ulaji wa safari hii wakubwa na jamaa zao wameamua kupiga trilioni…yaani trilioni. Bajeti za wizara kadhaa zimeishia mifukoni mwa watu. Mambo haya ukiyafikiria yanaweza kukutia wazimu,” alisema.
Akiwa mjini Tabora katika siku ya pili ya ziara hiyo, Mbowe aliitaka Serikali kuweka hadharani mkataba wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam na kuleta mkaguzi wa kimataifa kufanya uchunguzi katika tuhuma hizo nzito, ambazo alisisitiza kuwa zimevunja rekodi za kashfa mbalimbali za ufisadi kuwahi kutokea nchini.
Amshukia Sitta nyumbani kwake
Akiwa mjini Urambo katika mkutano wake wa jioni kati ya mikutano sita aliyofanya juzi, Mbowe aliwaambia wananchi kuwa, historia inayosimamia haki na matumaini ya Watanzania itakuja kumhukumu Samuel Sitta kwa maamuzi yake ambayo yamefanya Katiba Mpya na bora isipatikane mwaka huu kama walivyotegemea watu wengi.
Alisema kuwa maamuzi ya kibabe yaliyokuwa yakiibeba CCM katika Rasimu ya Katiba Mpya, yaliyofanywa na Sitta akiwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, yametoa fursa kwa wananchi kuunganisha nguvu zao sambamba na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kuanza mapambano mapya ya kudai Katiba Mpya inayotokana na maoni ya watu kwa ajili ya maslahi ya Watanzania wote.
“Wananchi wa Urambo, ndugu yenu alipewa mzigo mzito ukamshinda. Akatumia akili za ukada kufanya maamuzi ambayo yamefifisha ndoto za Watanzania kupata Katiba Mpya na bora kama walivyokuwa wakitarajia. Napenda kutumia fursa hii, kwa sababu nazungumza hapa Urambo, jirani kabisa na nyumbani kwake, kumwambia kuwa historia itamhukumu…
“Watanzania walikuwa na mategemeo makubwa ya kupata Katiba Mpya na bora inayotokana na maoni yao. Yeye kwa kuweka ukada mbele kwa ajili ya manufaa ya CCM, akasahau kuwa mchakato wa Katiba Mpya ni suala la muafaka wa kitaifa na maridhiano. Yeye akaweka chama chake mbele badala ya kuweka maslahi ya Watanzania mbele. Historia ya mapambano haya ya kudai haki na matumaini, itamhukumu huko mbele.
“Tunapenda kumwambia kuwa, mapambano ya kudai Katiba Mpya na bora ndiyo yameanza. Tumeidai kwa miaka 20 na zaidi, tutaidai hata kwa miaka 100 ijayo. Tena maamuzi yake ya kibabe, yametupatia fursa wapinzani kukaa chini na kuunganisha nguvu zetu kwa ajili ya upinzani wenye nguvu zaidi kuiondoa CCM madarakani,” alisema Mbowe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni