promotion

Jumatatu, 10 Novemba 2014

Mawaziri wamtosa Spika Makinda




BAADHI ya Mawaziri na Manaibu wao, wamekacha kuhudhuria hafla maalum ya kumpongeza Spika wa Bunge la Muungano, Anne Makinda, ambaye hivi karibuni alichaguliwa kwa kishindo kuwa Rais wa Bunge SADC kwa miaka miwili ijayo.
Halfa hiyo iliyoandaliwa na wabunge wanawake na kuwaalika mawaziri, viongozi wastaafu na wabunge wengine wote, ilifanyika katika viunga vya Bunge juzi, huku ikihudhuriwa na mawaziri wanne tu.
Mawaziri waliohudhuria hafla hiyo, ukiacha Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye aliwasili mapema katika viwanja hivyo, ni pamoja na Naibu Waziri Katiba na Sheria, Angela Kairuki, Waziri asiye na Wizara Maalum, Prof. Mark Mwandosya na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Spika wa Bunge wa zamani, Pius Msekwa, naye alikuwa miongoni mwa wachache wastaafu waliohudhuria sherehe hiyo.
Uchunguzi uliofanywa na Gazeti hili katika viwanja hivyo, ilibaini kuwa baadhi ya mawaziri hawakuwa na sababu ya msingi ya kutofika katika hafla hiyo ya kihistoria, kwani wengine walikuwa Dodoma Hotel wakiendelea kula na kunywa na wengine walikwenda kujirusha kwenye kumbi za burudani za mjini hapa na kukacha hafla ya Spika Makinda.
Ukiacha Mawaziri na Manaibu wao, wabunge wengi pia hawakuhudhuria hafla hiyo na hakuna sababu za msingi zilizotolewa za kutofika kwao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Spika Makinda, alisema hakutarajia kupata nafasi hiyo na siku zote anaamini kiongozi huchaguliwa na Mungu.
“Mimi naamini kiongozi anachaguliwa na Mungu kupitia watu wake. Kama hujachaguliwa, maana yake Mungu hajapenda, hivyo huna sababu ya kulalamika, kunung’unika. Kuna watu wanafikia hatua ya kunywa sumu kwa kukosa uongozi, kwanini ufanye yote hayo?,” alihoji Spika Makinda.
Alisema anachukua nafasi hiyo huku Bunge hilo likikabiliwa na changamoto lukuki za kiutendaji, ambazo nyingine ni za kimuundo, kiuchumi na za kimkakati.
“Bado kuna haja ya kutatua changamoto mbalimbali ndani ya Bunge letu hususani ukosefu wa namna bora ya kuwasilisha maamuzi ya Bunge hili ndani ya utaratibu wa Jumuiya ya Wanachama wa nchi za SADC, uwajibikaji hafifu kuhusu maamuzi ya Bunge hili kwa nchi wanachama, ukosefu wa namna bora ya kushirikiana na Bunge la Afrika, mawasiliano hafifu kati ya chombo hiki na mabunge ya nchi wanachama, uhaba wa rasilimali watu na fedha za kuendeshea chombo hiki,” alisema Makinda.
Aliwashukuru wabunge wote kwa kumpongeza na hasa wanawake, ambao walimkabidhi zawadi maalum kutokana na ushindi alioupata katika nafasi hiyo.
Waziri Mkuu Pinda, kwa upande wake alimpongeza Spika Makinda kwa nafasi hiyo na kwamba, ushindi alioupata ni sifa kwa Bunge la Tanzania na Tanzania kwa ujumla wake.
Makinda ambaye hakuwa na mshindani, alichaguliwa kushika nafasi hiyo wakati wa Mkutano wa 36 wa Bunge la SADC, ambalo linaundwa na mabunge ya nchi wanachama wa SADC (SADC PF), uliofanyika Hoteli ya Elephant Hill mjini Victoria Falls, Zimbabwe

Hakuna maoni: