Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema hana ugomvi na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kwa kuwa amemlea na amemesaidia vitu vingi zikiwamo fedha, gari, kula na kulala nyumbani kwake.
Mbowe alisema Chadema hakijamtenga Zitto bali alijitenga mwenyewe na kufafanua kuwa Chama hicho hakiwezi kujengwa na viongozi ambao ni wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aliyasema hayo jana katika Kata ya Kalinzi, Jimbo la Kigoma Kaskazini katika ziara zake za ‘operesheni delete CCM’ kuelimisha wananchi kuhusiana na uchaguzi wa serikali za mitaa na kuikataa Katiba iliyopendekezwa.
Mbowe alisema hayo baada ya kuruhusu maswali kutoka kwa wananchi ndipo Cheche wa Cheche alipomuuliza kwamba kwa nini Zitto hayumo katika ziara hiyo wala ya Katibu Mkuu, Dk.Willibrod Slaa.
“Kuna baadhi ya watu wanafikiri kuwa nampiga vita Zitto, siwezi kumpiga vita Zitto kwa kuwa nimemlea, amekula na kulala nyumbani kwangu nami ndie nilimshauri kugombea ubunge na kumpa fedha pamoja na gari, iweje leo nimpige vita?” alihoji Mbowe wakati akijibu swali hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni