Baadhi ya watu wakiangalia masalia ya basi la abiria la Wibonela baada ya kuondolewa sehemu lilipopata ajali eneo la Fantom Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga jana.(Picha: Mohab Dominick). |
Watu wanne wamefariki dunia papo hapo akiwamo mama mjamzito na kichanga baada ya basi walilokuwa wakisafiria kupinduka eneo la Phantom mjini Kahama mkoani Shinyanga.
Ajali hiyo iliyotokea jana asubuhi, iliambatana na tukio la wananchi kuua mtu mmoja wakimtuhumu kuwa kibaka aliyejaribu kuwapora fedha marehemu na majeruhi na ilihusisha basi la Wibonela Express lenye namba za usajili T412 CGN lililokuwa likisafiri kutoka Kahama kwenda jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo walisema ilitokea muda mfupi baada ya msafara wa mabasi mbalimbali kutoka katika Kituo Kikuu cha Mabasi Kahama kuelekea katika mikoa ya Singida, Dodoma na Dar es Salaam.
Basi hilo lililokuwa likiendeshwa na Godfrey Prochas, ambaye alikimbia baada ya ajali hiyo, inadaiwa alishindwa kumudu kukata kona na kusababisha basi hilo kuviringika na kupinduka.
Akizungumza eneo la tukio, Stanslaus Luhumbika, alisema basi hilo lilipinduka wakati likiingia barabara kuu ya kutoka Isaka kwenda Rusahunga, Rwanda likiwa katika mwendo kasi likifukuzana na mabasi mengine yaliyokuwa yameondoka kuwahi mizani ya Mwendakulima.
Mmoja wa majeruhi katika ajali hiyo mbaya kutokea mjini humu, Nickson Adadi (34), mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam ambaye amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama, alisema walianza safari saa 12:00 asubuhi, lakini walipofika kituo cha mafuta Phantom kuingia barabara kuu ya lami, alishindwa kulimudu basi hilo na kuserereka upande wa pili wa barabara na kupinduka.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Joseph Ngowi, alithibitisha kupokea miili minne ya abiria katika ajali hiyo akiwamo kichanga cha miezi mitatu, Robnic Jordan, huku wazazi wake wakijeruhiwa, mwili mwingine wa mama mjamzito aliyefahamika kwa jina moja la Amina, mkazi wa Kigoma.
Wengine waliofariki dunia ni Salum (35) na mmoja ambaye hajafahamika bado huku majeruhi wa ajali hiyo wakiwa 40, kati yao wanawake 14 na wanaume 26.
Ngowi aliwataja majeruhi hao ni Maulid Salum (40), mkazi wa Ushirombo, Emmanuel Lumbabo (34), mume wa marehemu Amina, Mchungaji Nickson Andart, raia wa Rwanda, Oscar Lameck (19) (Kigoma), Neema Dustan (18), Stahimili Shabaan (30), Happy David (32) wote wa Dodoma.
Wengine ni Iseme Ikila (36) (Katoro), Lucas Mlazi (48), Ibrahim Suga (30) (Kigoma), Agnes Groto (35) (Ngara), Tungu Lazaro (22, Bariadi), Kashinje Masanja (28, Ipoya Kahama), Frank Kishimba (21, Isaka), Athuman Issa (21), Jordan Mbuya (28), Blandina Patrick (24), Monica Gadson (35), Happy Hamisi, Everine Hamisi (6), Josephat Masha (19) wote wa mjini Kahama.
Mganga huyo aliwataja majeruhi wengine ni Jackson Hasauti (26, Kahama), Baligelea Ramadhan (40), Rita Brayson (25), Hamis Shaaban (31), Peter Bahati (22), Shaban Omari (16) wa Dodoma, Amicus Hamdun, Gloria Moses (18), Kulwa Said (40) na Peter Daud (42) wote wakiwa wakazi wa Kahama.
Mganga huyo aliwataja majeruhi wengine ambao majina yao hayajajulikana bado, akiwamo mtoto wa kike wa miaka sita hali zao ni mbaya na wamepelekwa hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza.
Alisema wengi wa majeruhi hao ambao wamelazwa hospitalini hapo wameumia sehemu mbalimbali za miili yao ikiwamo kichwani, miguuni, mikononi na kifuani, lakini wanaendelea kupata matibabu.
Wakati tukio hilo la ajali likitokea, lilitokea wimbi la vibaka ambao walijaribu kuwaibia majeruhi, lakini wasamaria wema walimnasa mara moja na kumsurubu na kumuua kisha kumchoma moto baada ya kubainika kuiba kompyuta mpakato na Sh. 800,000.
Ilidaiwa kuwa kibaka mwingine alikamatwa chumba cha maiti katika hospitali ya wilaya akipekua mifuko ya marehemu akijidai kuwatambua, na kutiwa mbaroni na kwamba anashikiliwa na polisi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kwamba dereva wa basi hilo anasakwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni