promotion

Jumanne, 25 Novemba 2014

Ndugai amenguliwa mjadala wa Escrow?


Safari ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai (Pichani), nje ya nchi imehusishwa na mpango wa kudhibiti mjadala bungeni unaohusu uchotwaji wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Habari za Ndugai kusafiri zilianza kuenea Alhamisi wiki iliyopita, huku zikidai kwamba, ni mikakati iliyopangwa dhidi yake kutokana na hatua yake ya kutaka ushauri kwa wabunge kuhusu nini kifanyike kuzuia mihimili mingine kuingilia utendaji wa Bunge.

 Ndugai alitoa fursa hiyo baada ya wabunge kuomba mfululizo miongozo ya Spika bungeni, kuhusiana na kashfa hiyo.

Wabunge walifikia hatua hiyo baada ya awali kuibuka madai na baadaye Bunge kukana kuhusu kuwapo kwa barua iliyoandikwa na Mahakama ya Tanzania, ikidaiwa kuzuia suala la Escrow kujadiliwa bungeni, kwa madai kwamba, lipo mahakamani.

Katika kuhitimisha ushauri aliopewa na wabunge wasiopungua saba, Ndugai aliahidi kutumia kanuni na sheria za Bunge ipasavyo na kusema atarejea misimamo ya aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samwel Sitta, kukataa umoja wa kulinda maovu.

Vyanzo mbalimbali vimedai kuwa baada ya jitihada za kumtaka Ndugai kusikiliza maelekezo kugonga mwamba, ndipo ikaamriwa asafiri kwenda nchini Uingereza kwa muda usiopungua siku 10.

Chanzo kinasema kuwa Ndugai amewekwa pembeni ili asisimie mjadala wa sakata hilo bungeni.

Taarifa zaidi zimedai kuwa Ndugai ameambiwa kuwa amepewa kazi maalum nje ya nchi ambayo ataifanya kwa siku 10 na atakaporejea atakuta mjadala wa Escrow bungeni umemalizika.

“Msimamo wake wa kusimamia suala hilo ili lijadiliwe bungeni na kutoa nafasi kwa wabunge wiki iliyopita kutoa ushauri kwa kiti cha Spika ndilo lililomponza,” kilieleza chanzo kimoja.

Vikao vya Bunge siku ya jana, viliendeshwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, ambaye kwa muda mrefu tangu Bunge lianze hakuwapo na inaelezwa kuwa ndiye tegemeo la wanaotaka mjadala huo udhibitiwe.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel, aliliambia NIPASHE jana kuwa, ingawa ni kweli Ndugai anasafiri, habari zinazohusisha safari yake na suala la Escrow bungeni ni za uzushi.

“Ni kweli Naibu anasafiri nje ya nchi, lakini kwamba ni kutokana na masuala ya uendeshaji wa vikao ni uzushi tu jamani, tena anaondoka kesho. Hebu mpigie yeye ndiye atawaeleza kwa uwazi kinachoendelea,” alisema Joel.

KAULI YA NDUGAI
Ndugai alipoulizwa na NIPASHE jana kuhusiana na taarifa hizo, hakupatikana. Hata hivyo, juzi jioni alipoulizwa, hakutaka kulizungumzia suala hilo zaidi ya kujibu kwa ufupi kupitia simu ya kiganjani:“Naomba jambo hili tuliache kama lilivyo.”

WABUNGE WANASEMAJE?
Baadhi ya wabunge waliozungumza na NIPASHE jana kuhusu fununu zinazohusu safari ya Ndugai namna anavyoongoza vikao vyao wakilinganisha na uongozi wa Makinda.

Kangi Lugola (Mwibara-CCM) alisema vikao vyote vya Bunge hutakiwa kuongozwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizoidhinishwabna kwamba, tatizo siyo Ndugai wala Makinda, bali ni wabunge wenyewe kuwa wanafiki.

“Kila mmoja lazima awe na tofauti na mwingine katika kutumia kanuni, kwa kuwa kila mmoja ana uwezo tofauti na mwingine katika kutumia na kutafsiri kanuni, hivyo ni jukumu la wanaoona tofauti kusema kwa wazi kuwa hakutendewa inavyotakiwa,” alieleza Lugora

Alisema Spika siyo mwenye mamlaka ya mwisho ya Bunge, bali wabunge wenyewe na kutaka wabunge watakaoona spika anapeleka Bunge ndivyo sivyo, wasimame bungeni na kuchukua hatua sitahiki siyo kulalamika pembeni.

Aliwataka kuiga kwake alipowasilisha hoja kuhusu kashfa ya oparesheni tokomeza kwamba alimudu kuzuia mipango ya kuipindisha mpaka haki ikatendeka.

Haroub Muhammed Shamis (Chonga-CUF) alisema kuna tofauti kubwa kati ya uendeshaji wa vikao kati ya Ndugai na Makinda, hali anayoihusisha na umri wao.na kuendelea kuongoza tofauti na mama ambaye anakaribia kustaafu,” alisema Shamis.

Tundu Lissu (Singida Mashariki-Chadema) alisema ingawa hafahamu lolote kuhusu safari ya Ndugai, suala la uendeshaji wa vikao vya Bunge lipo wazi na linafahamika na wabunge karibu wote.

“Kwenye masuala nyeti na ya msingi kama la Escrow, tabia ya Spika ni kuzima mjadala, wakati kwenye mambo ya msingi tabia ya Ndugai, ni kuruhusu mjadala, wako tofauti kabisa,” alisema Lissu.

MBINU CHAFU
Wakati hayo yakijiri, vitabu vyenye picha na magazeti yanayoeleza habari binafsi na kumshambulia Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, vilikuwa vikisambazwa na kugaiwa bure kwa wabunge bungeni.

Kusambazwa kwa vitabu hivyo na magazeti kunahusishwa na njama za kutaka kukwamisha mjadala bungeni kesho kuhusiana na ripoti ya uchunguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika akaunti ya Escrow.

NIPASHE  iliwashuhudia wabunge wakiwa na vitabu hivyo,  wakiwa wanasoma kwa kupokezana.Walioshuhudiwa ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Mbali na hao pia wabunge kadhaa walionekana wakiwa wameshika nakala ya kitabu hicho kilichosomeka ‘Mjue Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mtetezi wa Watanzania wanyonge’.

Katika kitabu hicho ambacho NIPASHE imefanikiwa kukiona na kukisoma, zimewekwa tuhuma kadhaa na masuala binafsi ya Zitto yanayoeleza namna anavyoshiriki wizi kwa kutumia watu katika maeneo mbalimbali.

Baadhi ya wabunge wa CCM na upinzani waliponda hatua hiyo na kusema ina lengo la kutaka kuzima mjadala wa uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Escrow.

Mbali na hilo, pia zilikuwa zikisambazwa nakala za gazeti moja la kila wiki (jina tunalo), ambalo lilikuwa na toleo maalumu, lililokuwa likigawiwa bure kwa wabunge na wageni mbalimbali.

Katika gazeti hilo, ambalo lilikuwa na kichwa cha habari kilichosomeka ‘Sakata la IPTL Zitto kuliingiza Bunge kwenye mtego wa hatari’.Gazeti hilo, ambalo Mwenyekiti wake wa bodi, Prince Bagenda, lina picha ya Zitto na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Lilikuwa likigawiwa na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Epson Kadya, ambaye ni meneja masoko na usambazaji wa gazeti hilo, ambaye alisema lengo la kugawa bure ni kutaka watu wajue ukweli kuhusu sakata hilo

WEREMA ATAHADHARISHA
Siku mbili kabla mjadala huo kutinga bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, amelitahadharisha Bunge kuwa makini katika kulijadili sakata la Escrow.

Akizungumza jana jioni bungeni wakati wa kufunga mjadala wa Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2014, alisema kwamba kwa sasa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) inafanya uchunguzi wa kimahakama, hivyo unatakiwa umakini.

“Nawaomba msichafuane katika mitandao, watu wameanza kulalamika kuhukumiwa kabla ya kusikilizwa,” alisema.
 


Hakuna maoni: