Mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kigezi iliyoko Chanika, wilayani Ilala, Dar es Salaam (jina linahifadhiwa), ameolewa na mkazi wa Mbondole, Halfa Ally (54) ambaye humfungia ndani ili wakazi wa eneo hilo wasimuone.
Mama wa mtoto huyo, alisema jana kuwa alipata taarifa kutoka kwa mdogo wake aliyekuwa akiishi eneo hilo kuwa mwanaye anaishi na mwanaume huyo zaidi ya mwezi mmoja na nusu na huwa anamfungia ndani ili asitoke nje.
Alisema mtoto huyo alikuwa anaishi na baba yake mzazi kwa zaidi ya mwezi mmoja eneo la Kivule, alishangaa kusikia kuwa mwanaye ameolewa na anaishi Mbondole.
“Nakumbuka ilikuwa Oktoba 7, mwaka huu tulitoa taarifa kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa, tulishirikiana na wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mtaa huo ambao tulifika eneo hilo saa moja asubuhi hadi saa 8 mchana na tulifanikiwa kumkamata mtuhumiwa,” alisema mama wa mtoto huyo.
Alisema walishangazwa na kitendo cha mwenyekiti wa serikali ya mtaa kumwachia huru mtuhumiwa bila kumchukulia hatua zaidi.
“Aliniambia tulimalize tu suala hili kienyeji ila niende duka la dawa nikanunue kipimo cha mimba ili tuangalie kama mtoto atakuwa kapata ujauzito na kama hana aendelee na shule.”
“Aliniambia tulimalize tu suala hili kienyeji ila niende duka la dawa nikanunue kipimo cha mimba ili tuangalie kama mtoto atakuwa kapata ujauzito na kama hana aendelee na shule.”
Mwenyekiti wa Mtaa huo, Salum Matangula alikiri kutokea kwa tukio hilo na alisema kilichotokea ni mtuhumiwa huyo alikiri mbele ya kikao kuwa alipewa ruhusa na mama mzazi wa mtoto huyo aishi naye.
Alisema kutokana na maelezo ya pande zote, walibaini wote wana makosa ndipo walipomtaka mama huyo aende kwenye duka la dawa ili achukuliwe kipimo cha mimba na baada ya hapo ampeleke mwanafunzi huyo shuleni.
“Niliwaeleza kuwa wote wana makosa, mama alikuwa anadai mwanaye akapime kwanza, nikamruhusu, lakini sijapata majibu hadi leo,” alisema Matangula.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kigezi, Joseph Kalungutu alisema mwanafunzi huyo ni mtoro na kipindi cha nyuma alikuwa akihudhuria darasani mara moja moja na lakini kuanzia Septemba, mwaka huu, hajaonekana kabisa shuleni.
“Mahudhurio ya mwanafunzi huyu ni mabaya, kuanzia Mei 14, mwaka huu hakuingia darasani lakini ilipofika Juni alionekana wiki moja, Julai alikuja siku mbili na Agosti aliingia darasani kwa siku nne tu,” alisema.
Mwanafunzi huyo alisema waliishi na mwanaume huyo kuanzia Septemba, mwaka huu, baada ya kuchukuliwa nyumbani alikokuwa anaishi na baba yake mzazi eneo la Kivule.
“Alinichukua kama mke wake na kuniambia kuwa ninaenda kwake kumlelea watoto wake watatu ambao walikuwa hawana mlezi,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki alisema hajapata taarifa hiyo na kuahidi kufuatilia ili mtuhumiwa afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Ally alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo, alisema ni kweli msichana huyo anamfahamu na alikuwa anaishi naye. “Sina cha kukueleza zaidi ya hayo ninachofahamu huyo binti nilikuwa naishi naye,” alisema Ally.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni