promotion

Jumatano, 29 Oktoba 2014

Kesi ya Kulawiti na Kutuma Picha Katika Mitandao ya Kijamii inayowakabili Watu Wawili





SHAHIDI wa kwanza katika kesi ya kulawiti na kutuma picha katika mitandao ya kijamii inayowakabili wakazi wawili wa Mbagala, Dar es Salaam, alidai kwamba alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mlalamikaji kwa miaka saba huku akiwa na mume wake ambaye ni mshitakiwa namba moja katika kesi hiyo.

Sanifa Sadick alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi Saidi Mkasiwa kuwa mshitakiwa Erick Kasira (39) ni mume wake tangu mwaka 2006 na kwamba wana watoto wawili huku mshitakiwa wa pili, Juma Richard ni shemeji yake.

Alidai kwamba Agosti 23 mwaka huu, waliwasiliana na mlalamikaji huyo ili wakutane katika nyumba ya kulala wageni inayojulikana kama Maembe Bar & Guest House iliyopo Yombo Kiwalani kwa ahadi ya kusaidiwa Sh 100,000.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto, shahidi huyo alidai muda wa saa 7 mchana alimuaga mume wake kwamba anaenda kununua bidhaa za saluni.
Alidai kwamba alichukua usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda huku mlalamikaji akimuelekeza kwa njia ya simu.

Sanifa alidai kwamba wakati anaelekea Yombo kulikuwa na mwendesha pikipiki ambaye alikuwa anamfuatilia kwa nyuma hadi eneo hilo.

Alidai kwamba alimkuta mlalamikaji akiwa peke yake na kuagiza kinywaji baadaye walichukua chumba namba sita na kuingia ndani; baada ya muda mlango wa chumba hicho uligonjwa ndipo alimuona mumewe akiingia pamoja na vijana watatu.

‘’Sikuweza kuwatambua wote lakini hawakuwa na silaha zaidi ya simu. Mpenzi wangu aliulizwa na mume wangu kuwa anafanya nini na mimi, naye alimjibu kuwa asiniache kwani atampa gharama yoyote ndipo waliandikishiana kutoa Sh 500,000 ,’’ alidai Sanifa.

Alieleza mlalamikaji kuwa alikuwa na kompyuta na kwamba alimwambia Erick akae nayo hadi atakapompatia fedha hizo walizoahidiana.

Alidai kwamba alikuwa amejificha chooni na kusikia kwamba wanaume hao wanamtaka mlalamikaji afanyiwe kinyume na maumbile na kwamba walimvua nguo zote huku aliyekuwa mwendesha bodaboda akiwa anapiga picha.

Alidai baada ya tukio hilo alikimbilia nyumbani na kukuta simu aina ya Tecno nyumbani kwake na kuiweka laini yake baadaye dada yake alimtumia picha ikimuonesha mlalamikaji akiwa utupu.

Alieleza kwamba mlalamikaji alimpigia simu Erick na kumwambia aende akachukue fedha alizoahidi kutoa wakati akifumaniwa na mke wa mshitakiwa huyo na kwamba mshitakiwa huyo aliondoka pamoja na ndugu yake Richard.

Alidai walipofika Tandika, waliwekwa chini ya ulinzi na Erick alimpigia simu mkewe kumtaarifu kwamba amekamatwa na polisi naye alipofika aliwekwa chini ya ulinzi. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 3 mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa.

CHANZO: Habari Leo.

Hakuna maoni: