Mbunge huyo anayesifika kwa kujenga hoja bungeni, anahoji wanapokwenda nusu ya wanafunzi wanaomaliza shule kila mwaka na kushindwa kuendelea na masomo.PICHA|MAKTABA
Kila baada ya matokeo ya mitihani ya taifa kutolewa, taifa hugubikwa na mijadala mingi kuhusu hali ya elimu nchini.
Hata hivyo, mijadala hiyo hupita kama upepo, japo mara nyingi matokeo hayo huacha simanzi kubwa kuhusu hali halisi ya sekta ya elimu ilivyo nchini.
Ni simanzi itokanayo na matokeo mabaya ambayo pia yanaonyesha kuwepo kwa walakini katika sekta ya elimu.
Walakini huu kwa mujibu wa mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe haujatafutiwa mwarobaini na kibaya zaidi haoni jitihada zozote za dhati za kurekebisha hali ya mambo kabla hayajaharibika.
“Kwa jumla, sekta ya elimu imetelekezwa na watu wanazungumza kama elimu haina mwenyewe. Iko haja ya kuzungumza kwa umakini kabla mambo hayajaharibika kabisa,’’ anasema.
“Tunahitaji kuhakikisha kwamba kuna usimamizi mzuri katika elimu. Hivi sasa yanatoka matokeo mabaya kidato cha nne au sita watu wanapiga kelele, lakini baada ya wiki tunaendelea na maisha kama kawaida.”
Zitto, mbunge kijana aliyejizolea sifa kubwa katika duru za siasa nchini, anasema hali duni ya elimu inajidhihirisha katika shule za umma ambazo miaka ya nyuma zilikuwa kimbilio la wengi, lakini sasa zinakimbiwa.
Enzi hizo, anasema Zitto kuwa wazazi walifikia hatua ya kufanya hila na udanganyifu, alimradi watoto wao wasome katika shule hizo zilizokuwa zikitamba kwa taaluma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni