promotion

Jumatatu, 25 Agosti 2014

Mtikila: Mgombea binafsi mwiba kwa serikali




































MWENYEKITI wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amesema Serikali inaangaika kutekeleza hukumu ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu ya kutaka suala la mgombea binafsi liwemo katika Katiba.
Alisema kuwa hatua hiyo ndiyo inaifanya serikali kutaka kufanya mabadiliko katika katiba ya sasa ili kuweka suala hilo endapo mchakato wa kupata katiba mpya utashindikana kabla ya uchaguzi mkuu.
Hivi karibuni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa hofu ya kutopata idadi kamili ya wajumbe wa kutimiza theuluthi mbili ya kura za Bunge Maalum la Katiba, watalazimika kurudi katika Bunge la kawaida.
Werema alisema kuwa katika Bunge hilo la kawaida watafanya mabadiliko ya 15 hasa kuhusiana na vipengele vya muhimu ikiwemo mgombea binafsi, mamlaka ya Rais, Tume ya Uchaguzi na mengineyo.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, mchungaji Mtikila alisema kuwa serikali imekosa lugha ya kutumia katika kutekeleza suala la mgombea binafsi ndiyo maana imekuwa ikiangaika namna ya kufanikisha suala hilo.
Mtikila alisema kuwa serikali ilipewa miezi sita kuhakikisha suala la mgombea binafsi linakuwepo katika Katiba, kwamba hata baada ya kubaini Katiba mpya haiwezi kupatikana wanalazimika kukimbilia kutekeleza hilo Bunge la kawaida.
“Hili suala la mgombea binafsi ni mwiba kwa serikali ni hukumu ndiyo inayotaka waitekeleze na hadi sasa imebaki miezi mitatu ambapo watatakiwa kuwasilisha ripoti katika mahakama hiyo kuonyesha namna walivyotekeleza suala hilo,” alisema.
Alisema kuwa anaamini serikali inaangaika kujinasua kuonyesha kuwa wametekeleza hukumu hiyo na hata liwepo katika uchaguzi mkuu ujao wa mwakani.
“Wanachotaka kukifanya Werema na wenzake ni kutaka kuonyesha kama wao ndiyo wanawapa haki Watanzania lakini ukweli ni kuwa wanaitekeleza ile hukumu tena na muda uliobaki ni mchache kwani inatakiwa kuonekana kikatiba,” alisema.


Mwaka 1993, Mchungaji Mtikila alifungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma iliyosikilizwa na Jaji Kawha Lugakingira ambaye alikubaliana na hoja zake, kwamba kugombea kama mtu binafsi ni haki ya kila raia kwa mujibu wa Katiba, kwa maana ya haki ya kuchagua viongozi na haki ya kugombea uongozi.

Hakuna maoni: