promotion

Jumatatu, 25 Agosti 2014

Askofu Mukuta anatarajiwa kuzikwa Jumanne




































ASKOFU wa kwanza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Paulo Mukuta, atazikwa Jumanne Agosti 26 mwaka huu, katika viwanja vya Kanisa Kuu la Lukajange.
Askofu Mukuta alifariki dunia Afosti 19 mwaka huu, katika hospitali ya KCMC mjini Moshi. Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Askofu wa sasa wa Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza, ilisema kuwa Askofu Mukuta atazikwa kwa heshima zote za kanisa hilo.
Mwili wa hayati Askofu Mukuta utawasili uwanja wa ndege wa Karagwe/Ihanda ukitokea Moshi na kupokelewa na waumini kabla ya kufikishwa nyumbani kwake katika kijiji cha Nyakahanga.
Ratiba ya shughuli za mazishi inaonyesha kuwa baada ya ibada fupi nyumbani kwa Askofu Mukuta, mwili utahifadhiwa katika hospitali ya Nyakahanga kusubiri mazishi siku ya Jumanne.
Aidha, ratiba hiyo inaonyesha kuwa mwili wa hayati Askofu Mukuta utahamishiwa katika Kanisa Kuu siku ya Jumatatu kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho na utalala humo katika mkesha maalum.
Ibada ya Mazishi itaongozwa na Mkuu wa KKKT, Askofu Dk. Alex Malasusa atakayeongozana na maaskofu wengine kutoka dayosisi mbalimbali za kanisa hilo.
Askofu Paulo Mukuta aliongoza dayosisi ya Karagwe tangu mwaka 1979 hadi 1996 alipostaafu.
Chini ya uongozi wake, shule ya kwanza ya sekondari ilijengwa wilayani humo. Dayosisi ya Karagwe ambayo hivi inaongozwa na Askofu Bagonza, inamiliki na kuendesha shule mbalimbali, hospitali teule ya wilaya, miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii na hivi sasa inajenga Chuo Kikuu cha Kilimo na Stadi za Mazingira.
Dayosisi ya Karagwe ilizinduliwa Januari 1979, ikimegwa kutoka Dayosisi ya Kaskazini Magharibi yenye makao Makuu mjini Bukoba. Dayosisi ya Karagwe inajumuisha wilaya za Ngara, Karagwe na Kyerwa.
Kabla ya kuchaguliwa kuwa Askofu wa Karagwe, Askofu Mukuta alifanya kazi za kichungaji katika maeneo ya Kyaka, Ndolage na Ofisi Kuu ya dayosisi mjini Bukoba. Amefariki akiwa na umri wa miaka 78, ameacha mjane na watoto 5.

Hakuna maoni: