Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa amefariki dunia baada ya kuanguka ghafla kutoka kwenye kiti alichoketi wakati akishiriki Kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Tarime.
Taarifa kutoka ndani ya kikao zilidai kuwa kabla ya kufikwa na mauti, Tuppa alisalimiana na wajumbe wa kamati hiyo kabla ya kuanza kwa kikao.
Baada ya kuanguka alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime, ambako alifariki dunia wakati akipewa matibabu.
Kikao hicho kilikuwa maandalizi ya kukabidhi vyeti kwa vijana waliomaliza mafunzo ya mgambo Kijiji cha Nyamwaga, wilayani Tarime. Mafunzo hayo yameandaliwa na Kikundi cha Ulinzi cha Nyabigena Security Cooperative Ltd.
Akitangaza kifo hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Bendicto ole Kuyani alisema Tuppa alionekana mwenye afya njema jana asubuhi kabla ya kuelekea Tarime kikazi.
Kuyani alisema Tuppa hakuwa na historia ya kusumbuliwa na ugonjwa wowote, ingawa taarifa zisizo rasmi zinadai kuwa chanzo cha kifo ni shinikizo la damu.
Daktari athibitisha:
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime, Dk. Nega Nyakabogo alithibitisha kifo hicho. “Tulimpokea akiwa kwenye hali mbaya, jitihada za kuokoa maisha yake zilishindikana,” alisema Nyakabogo.
Hata hivyo, Dk. Nyakabogo hakuweka wazi chanzo cha kifo hicho na kusema mwenye nafasi ya kuzungumza zaidi ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime.
Kikwete atuma rambirambi:
Wakati huohuo, Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia kufuatia kifo hicho.
“Pokea rambirambi zangu za dhati na masikitiko makubwa kufuatia kifo cha John Gabriel Tuppa. Ni huzuni kubwa na pigo kwa Serikali na hasa kwa watendaji wenzake mkoani Mara,” ilisema sehemu ya taarifa ya Rais Kikwete iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni