MKUU wa Mkoa wa Mara, John Tuppa, amefariki dunia jana akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Tarime.
Taarifa za kifo chake zilitolewa kwa waandishi wa habari na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele, ambapo alisema marehemu alikwenda ofisini kwake (Henjewele) kwa ajili ya shughuli za kikazi.
Alisema marehemu alikuwa na ziara ya kwenda kufungua ofisi ya mgambo katika Kijiji cha Nyamwaga lakini alipokuwa ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime kwa ajili ya maandalizi alianguka chini na baadaye kupoteza fahamu.
“Mkuu wetu wa mkoa amefariki dunia leo, tupo kwenye taratibu nyingine za msiba huu… mwili wake tumeutoa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime na kuufikisha mjini Musoma,’’ alisema Henjewele.
Henjewele alisema marehemu baada ya kuanguka chini ofisini kwake alipoteza fahamu na kisha kukimbizwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa matibabu zaidi.
Alisema kuwa marehemu Tuppa alipoteza maisha muda mfupi baada ya kupewa huduma ya matibabu.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, Robert Onesmo, alisema marehemu Tuppa alifariki dunia kutokana na tatizo la maradhi ya kiharusi.
Alisema matatizo hayo yalibainika baada ya madaktari kumfanyia uchunguzi marehemu mara baada ya kufikishwa hospitalini hapo.
Naye Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine, alisema Mkoa wa Mara umepata pigo kubwa kutokana na kifo hicho lakini aliwataka wana familia na wananchi kuwa wavumilivu.
“Ninaungana na familia, wananchi na viongozi wote wa serikali za wilaya zote za wilaya za Mkoa wa Mara kuomboleza kifo cha Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa,’’ alisema.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Amos Sagara, alisema kifo hicho ni pigo kubwa, kwakuwa marehemu Tuppa alitoa msukumo mkubwa katika utekelezaji wa fedha za miradi ya maendeleo.
Ikulu yaomboleza
Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia, kutokana na kifo hicho.
Katika taarifa yake iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, Rais Kikwete alisema amepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Tuppa, ambaye alikuwa akifanya kazi mkoani Mara.
Ikulu, Rais Kikwete alisema amepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Tuppa, ambaye alikuwa akifanya kazi mkoani Mara.
Rais Kikwete alimuomba Waziri Ghasia amfikishie salamu za pole kwa mke wa marehemu, watoto na familia ya Tuppa kwa kuondokewa na kipenzi chao.
Alibainisha kuwa anaelewa machungu wanayoyapitia katika kipindi hiki kigumu, kwani wamepoteza nguzo imara waliyokuwa wakiitegemea katika maisha yao.
“Hakika tumempoteza kiongozi mchapa kazi ambaye amekuwa akijituma na kuwatumikia wananchi wake hadi dakika za mwisho za uhai wake. Pengo aliloliacha marehemu Tuppa haliwezi kuzibika kamwe, lakini hatuna budi kumwombea kwa Mwenyezi Mungu kuipumzisha roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.” Ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni