mcharoman blog fahar yako mtanzania
SOURCE EDDY BLOG
SERIKALI imekanusha uvumi uliozagaa katika mitandao ya jamii wiki hii kuwa wanyama aina ya twiga wanatoroshwa kutoka pori tengefu la Loliondo na kupelekwa nje ya nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara Maliasili na Utalii, Dkt. Adelhelm Meru (Pichani) ameziita habari hizo kuwa za uongo, uzushi na uchochezi.
Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Dkt. Meru alisema jambo hilo si la kweli na linalenga kuleta chuki dhidi ya serikali.
“Picha zile zimetolewa katika intaneti na kuelezwa kuwa ni za Tanzania, si kweli. Ni picha za kughushi,” alisema Dkt Meru.
Pia alibainisha kwamba twiga wa Tanzania wanatumika kama nembo ya taifa na hawaruhusiwi kuwindwa hata kidogo, “sasa kusema wamewindwa na kusafirishwa ni uzushi na upotoshaji.”
Alisema ukweli uliopo ni kwamba Kampuni ya Ortero Business Corporation iliyosajiliwa hapa nchini iliomba kibali cha kawaida cha uwindaji na kukubaliwa.
Kampuni hiyo ilipata vibali vya watu wanane vya uwindaji wa wanyama wakiwemo kongoni, ngiri, pofu, na swala pamoja na aina ya ndege mbalimbali. Kibali hakikuhusisha wanyama kama twiga, simba wala tembo.
Alisema kufuatia kibali hicho tarehe 25 Septemba, 2015 zilikuja ndege tatu aina ya CI 30 UAS, 312, na kupata kibali namba TCAA/5055/21294 ya mizigo; ndege ya abiria L6RJI iliyopata kibali namba TCAA/5055/21295 na ndege nyingine ya abiria A9HRM 767 iliyopata kibali namba TCAA/5055/21300.
Ndege hizo zilikuwa na Mohamed Sheikh Mohamed Bin Rashid, Mfalme toka Umoja wa nchi za Falme za Kiarabu akiambatana na msafara wa watu 137 na kutua katika uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA).
Alisema ujumbe huo wa watu ulifuata taratibu za kuingia nchini na kupata vibali halali vikiwemo vya uhamiaji na baadaye walielekea Loliondo.
Miongoni mwa watu hao walikuwemo watazamaji, wafanyakazi wa ndege hizo, watoa huduma wa mfalme huyo miongoni mwa wengine.
Alisema vibali vya uwindaji huo vimeipatia serikali dola za kimarekani 41,400 sawa na Tshs milioni 85.
Kwa mujibu wa Dkt. Meru, baadhi ya watalii hao pamoja na mfalme huyo waliondoka Septemba 29, 2015 huku baadhi ya maofisa wake wakiwa bado hapa nchini kwa ajili ya kukamilisha utaratibu wa kuhakiki wanyama na ndege waliowindwa na malipo ya serikali.
Dkt. Meru alisema uwindaji huo ulisimamiwa na maofisa wa jeshi la polisi, usalama wa taifa, maofisa wa kuzuia wanyama wanaokatazwa kuwindwa, maofisa wa halmashauri ya Loliondo na maafisa wa wizara kitengo cha kuzuia ujangili.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Bw. Herman Keraryo utalii wa kuwinda ni moja ya vyanzo vikubwa vya mapato si kwa Tanzania tu bali na nchi nyingine duniani.
Kwa mwaka jana tu, utaliihuo uliingizia Wizara dola za Kimarekani milioni 18.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni