promotion

Jumamosi, 29 Agosti 2015

BABU AWAMWAGIA MAJI YA MOTO WAJUU ZAKE 3, MMOJA AFARIKI DUNIA...SIMIYU"

mcharoman blogy fahar yako mtanzania
Mama wa mtoto aliyemwagiwa maji na kupoteza maisha Bi kundi kulwa akielezea waandishi wa habari(hawapo pichani) kilichotokea
FAMILIA YAFICHA TUKIO KWA MWEZI MZIMA, WAZAZI WAPOZWA KWA MBUZI WATANO.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida Mtoto mwenye umri wa miaka (3) (jina linahifadhiwa) amefanyiwa ukatili wa kinyama baada ya kumwagiwa maji ya moto na Babu yake Ilanga Kapolu (58) na kufariki dunia.

Babu huyo ilidaiwa kuwamwagia watoto wengine wawili ambao wamebaki na majeraha makubwa mwilini kwao, huku tukio hilo likifichwa na wazazi wa watoto pamoja na ndugu wa familia hiyo kwa muda wa mwezi mmoja.

Tukio hilo inadawa kutokea mwezi julai mwaka huu katika Kijiji cha Mwakasanda kata Bumela katika wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu, huku chanzo kikielezwa kuwa ni ulevi.


Baada ya tukio hilo kutokea na kufichwa ndani ya familia, baadhi ya wananchi katika kijiji hicho walitoa taarifa kwa waandishi wa habari hali iliyopelekea kufanyika uchunguzi wa kina juu ya ukweli wa tukio hilo.

Katika uchunguzi huo mama mzazi wa mtoto huyo aliyefariki ( kundi Kulwa) alidhibitisha kutokea kwa tukio hilo, sambamba na kukiri kufichwa ili lisijulikane baada ya kutishiwa maisha na Babu huyo.

Akieleza mazingira ya tukio zima Kulwa alisema kuwa Baba mkwe wake (Ilanga Kaporu) siku ya tukio alifika nyumbani akiwa amelewa na kumkuta akiwa na watoto hao wanapika chakula cha usiku.

‘’siku ya tukio baba mkwe alinikuta nikiwa na watoto wote watatu….akauliza bado haujapika?….nikamwambia ndiyo nimeinjika maji ya ugali….baadaye nikamuaga kufuata unga dukani….niliporudi nikakuta watoto wote wamemwagiwa maji ya moto” Alisema kulwa na kuongeza

“kati ya watoto hao mmoja alikuwa wa kwangu ambaye alifariki baada ya kuunguzwa sana…..na wengine wawili walikuwa ni watoto wake.....na waliunguzwa sehemu za kifua, mapaja, miguu, mgongo na matako hali iliyosababisha mwanangu kupoteza maisha’’

Kulwa alieleza kuwa wakati wa tukio mme wake hakuwepo nyumbani, ambapo alipiga yowe ili kuwaita majirani kushuhudia tukio hilo na kuweza kutoa msaada wa kuweza kuwakimbiza watoto hao hospitali.

Alieleza kuwa mzee Kapolu licha ya kuwajeruhi watoto hao alikataa kupelekwa hospitali na badala yake watumie dawa za miti shamba ili kuweza kuwatibu vidonda vya majeraha walivyokuwanavyo.
 
“ majirani pamoja na mme wangu walishindwa kutoa msaada baada ya kufika kutokana na kumwogopa mzee….watoto walikaa ndani wakiwa na majeraha makubwa….na baada ya siku mbili mtoto wangu akafariki kutokana na kuumia zaidi na kukosa matibabu”.

Kija Kishepo ambaye ni Bibi wa marehemu alisema kuwa baada ya mtoto kufariki, walipigiwa simu usiku na asubuhi walipofika walikuta taratibu zote za mazishi zimekamilika.

Alisema baada ya kushiriki mazishi ndipo walipopata taarifa kutoka kwa majirani juu ya kifo cha mjukuu wao, ambapo waliamua kuhoji kama ni kweli na kutaka kupewa ufafanuzi wa kina chanzo cha tukio.

“ Baada ya sisi kugundua familia zote mbili zilikaa kikao siku ya mazishi….na sisi tulitaka kuchukua hatua za kisheria kuripoti polisi….lakini katika kikao hicho Yule mzee alikiri kutenda kosa hilo….ambapo aliomba msaama na kutozwa faini mbuzi watano” Alisema Kishepo.

Kwa upande wake Kishepo Kulwa mke wake Kija alisema kuwa baada ya mzee huyo kukiri kutenda kosa hilo familia iliamua kumtoza faini ya mbuzi watano, huku wakitakiwa kutotoa taarifa za tukio hilo katika ngazi yeyote ya serikali.

“kutokana na ushauri wa ndugu na jamaa, mzee huyo alitozwa faini ya mbuzi watano lakini mimi sikufurahishwa na kitendo kile ikanilazimu kuuchukua binti yangu na kurudi nae nyumbani baada ya kuona maisha yake yako hatarini” Alisema Kishepo

Hata hivyo baadhi ya majirani ambao hawakutaka kutajwa kwa majina yao walisema kuwa kitendo kilichofanya na mzee huyo ni ukatili mkubwa ambao haupaswi kufumbiwa macho na jamii.

Waliongeza kuwa wanashangazwa kuona familia iliyotendewa kitendo hicho kukaa kimya, akiwemo Baba na mama wa marehemu, bila ya kutoa taarifa katika ngazi za kisheria ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.

“ kitendo hiki hakikubaliki hata kidogo ni ukatili wa hali ya juu tunaomba vyombo vinavyohusika kumchukulia hatua Babu huyo…..lakini tunaiomba familia kuacha kuogopa na badala yake watoe taarifa” Alisema

Alipotafutwa mtuhumiwa wa ukatili huo (Ilanga Kapolo) hakuweza kupatika hata nyumbani kwake, huku majirani wakieleza kuwa alitoweka kusikojulikana pamoja na familia yake.

Mbali na hilo mtuhumiwa huyo ilibainika kuwa watoto ambao walibaki na majeraha baada ya kumwagiwa na maji hayo, walifichwa kusikojulikana baada ya kupewa taarifa kuwa tukio limejulikana kwa wananchi wa kijiji hicho.

Hata hivyo katika hali ya kushangaza uongozi wa Kijiji hicho chini ya mwenyekiti wake Mkwabi Salu alipoulizwa juu ya kupata taarifa za tukio hilo alisema kuwa yeye hana taarifa.

Mwenyekiti huyo mbali na kukiri kutokea msiba wa mtoto katika familia hiyo ambapo alishiriki kuhudhulia mazishi yake, alieleza kuwa hajapata taarifa juu ya chanzo cha kifo cha mtoto huyo.

“ ni kweli kulitokea msiba wa mtoto katika familia ya mzee Kapolo….na mimi nilishiriki mazishi ya msiba huo….lakini taarifa za kuwa kifo cha mtoto huyo kilisababishwa na kumwagiwa maji bado sijazipata na sasa zimepita wiki mbili” Alisema Salu.

Katika uchunguzi huo ilibainika kuwa mtuhumiwa huyo Ilanga aliitwa katika uongozi wa askari wa kijadi (sungusungu) na kupewa adhabu kwa kupigwa viboko kutokana na kitendo alichokifanya.

Aliotafutwa Kamanda wa Sungusungu  Masanja Nyalandu alisema kuwa alipata taarifa kutoka kwa wakazi wa kijiji hicho juu ya tukio hilo, ambapo alikana kuwa sungusungu kumwazibu mtuhumiwa kutokana na kosa hilo”

“ ni kweli jana tumekaa kikaa na sungusungu wangu….tulimuita huyo mzee lakini kulikuwepo na mashataka mengine ya kutukana watu ndiyo maana tukamwazibu…siyo kweli kuwa adhabu hiyo ni kwa sababu ya tukio hilo….inagawa niliata taarifa zake” Alisema Nyalandu

Kwa upande wake diwani wa kata hiyo Mboje Muli alisema kuwa ofisi yake ya kata haina taarifa juu ya tukio hilo, huku akihaidi kulifanyia kazi ili kujua ukweli wake.

“ kwanza nawashukuru waandishi wa habari kwa kunipatia taarifa hizi…na mimi nashangaa kuletewa taarifa hizi na nyie sisi ambao tuko huku hatulifahamu hata kidogo….naomba nipewe muda nilifanyie kazi” Alisema Muli.

Mbali na tukio hilo kuripotiwa kwa waandishi wa habari bado katika ngazi za kitongoji, kijiji, kata, wilaya na hata polisi halijaweza kuripotiwa baada ya wahusika kutishiwa maisha na kutakiwa kukaa kimya.

Habari na. Derick Milton Simiyu.


Hakuna maoni: