mcharoman blogy fahar yako mtanzania
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amekana kumtolea lugha chafu Askofu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wakati akisomewa maelezo ya awali katika Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam jana.
Akisomewa maelezo na Wakili wa Serikali, Joseph Maugo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilfred Dyansobera, Gwajima alikana kutoa lugha chafu ila alikubali kuwa yeye ni askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, majina yake na kwamba aliitwa polisi Machi 27, 2015 kwa ajili ya kuhojiwa .
Maugo alidai upande wa mashtaka utawaita mashahidi saba kutoa ushahidi dhidi ya Gwajima pamoja na kuwasilisha vielelezo vitano.
Wakili wa Gwajima, Peter Kibatala aliomba kupewa maelezo ya mlalamikaji katika kesi hiyo.
Hakimu Dyansobera aliuagiza upande wa mashtaka kuwapatia maelezo ya mlalamikaji na kwamba kesi itaanza kusikilizwa kwa mashahidi upande wa mashtaka kutoa maelezo yao Agosti 10, mwaka huu.
Ilidaiwa kuwa kati ya Machi 16 na 25, mwaka huu kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, Gwajima alitoa lugha chafu dhidi ya Pengo.
Akisoma maelezo ya awali, Maugo alidai kati ya Machi 16 na 25, Gwajima alitoa maneno machafu kwa Pengo.
Hata hivyo, Gwajima aliyakana maelezo hayo na kukubali maelezo yake binafsi ya kuitwa polisi.
Katika kesi inayomkabili Askofu Gwajima na wenzake watatu, Maugo alisema nayo ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali, lakini mshtakiwa mmoja hakuwapo mahakamani kutokana na kusumbuliwa na maradhi.
Alidai kwa mujibu wa sheria, mshtakiwa anatakiwa kuwapo mahakamani, hivyo aliomba ipangwe tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali, ambapo itasikilizwa Oktoba 8, mwaka huu.
Katika kesi hiyo, Gwajima anakabiliwa na shtaka la kushindwa kuhifadhi silaha na risasi anazomiliki kihalali.
Kwa upande wa washtakiwa wenzake, akiwamo mlinzi wake, George Mzava, Yekonia Bihagaze na Mchungaji Georgey Milulu, wao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa wakimiliki bastola aina ya Berretta pamoja na risasi 20 kinyume cha sheria.
Wanadaiwa kuwa Machi 29, mwaka huu katika Hospitali ya TMJ, Mikocheni A walikutwa wakimiliki bastola hiyo yenye namba CAT 5802 bila ya kuwa na kibali kutoka mamlaka husika.
Pia wanadaiwa kuwa siku hiyo, washtakiwa hao pia walikutwa wakimiliki isivyo halali risasi tatu za bastola pamoja na risasi 17 za bunduki aina ya Shotgun. Washtakiwa wako nje kwa dhamana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni