promotion

Jumamosi, 27 Juni 2015

Serikali yaondoa Muswada wa Habari bungeni.

mcharoman blogy fahar yako mtanzania
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Mark Mwandosya.


Hatimaye serikali imeondoa Muswada wa Sheria ya Haki ya upatikanaji habari wa mwaka 2015, uliokuwa usomwe kwa mara ya pili leo na badala yake utasomwa katika Bunge la kwanza la serikali ijayo. 
 
Akitoa taarifa ya kuondolewa kwa Muswada huo jana bungeni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Mark Mwandosya, alisema Muswada huo ulichapishwa Februari 20, 2015 na kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni Machi 12, hadi Aprili Mosi, mwaka huu.
 
"Mheshimiwa Naibu Spika huu si muswada wa dharura kama ambavyo wengine wanazungumza,"alisema.
 
Alisema kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, iliyokutana Juni 22, mwaka huu ilijadili kwa kina Muswada huo na kuzingatia maoni ya wadau wa tasnia hiyo na kushauri kuwa inahitaji muda zaidi kuujadili na kuendelea kupata maoni zaidi ya wadau.
 
"Serikali imetafakari maoni ya kamati na kuafiki muswada uendelee kufanyiwa kazi hadi hapo kamati itakapokamilisha kazi yake ipasavyo na kuwakilisha maoni yake bungeni,"alisema.
 
Alisema matarajio ni kwamba muswada huo utasomwa kwa mara ya pili na ya tatu katika bunge lijalo.
 
Juni 22, mwaka huu, wadau mbalimbali wa habari, waliokutana mjini Dar es Salaam  walipinga muswada huo, kwa kile kinachoelezwa kuwa unakiuka sheria za kimataifa, Katiba ya nchi na kuwanyima haki raia kupata taarifa na kuua ndoto ya vijana wanaotarajia kunufaika na tasnia ya habari.
 
Wadau hao ni Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania ( Moat), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa) Tawi la Tanzania na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).
 
Mmiliki wa Kampuni ya New Habari Cooperation, Rostam Aziz, alisema muswada huo ni mbaya kwani unazuia dhana nzima ya uwazi na ukweli hivyo kulirudisha taifa nyuma na kuitaka serikali kutopeleka bungeni hadi wadau wote wa tasnia ya habari watakapotoa maoni.
 
Akitangaza maazimio ya mkutano wa Moat na wadau, Mwenyekiti wa Moat, Dk. Reginald Mengi, alisema kupitishwa kwa muswada huo kutawanyima uhuru wa usambazaji wa habari kwa vyombo vinavyomilikiwa na watu binafsi jambo ambalo ni kinyume cha katiba ya nchi.
 
Dk. Mengi alieleza kushangazwa na utungwaji wa sheria hiyo ambayo kwa upande mmoja inatambua na kuheshimu misingi ya katiba katika ibara ya 5 na upande mwingine ibara ya 18 ikikataza taarifa iliyotolewa chini ya ibara ya 5 (1) kwa umma na kutoa vitisho kwa atakayekiuka na kupatikana na hatia ya kufungwa kifungo cha miaka isiyopungua mitano jela.
MCT WAPINGA
 
Akizungumza na waandishi mjini Dodoma, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema baraza hilo limetoa ombi hilo kwa sababu wadau wa habari hawakuwa na muda wa kutosha kutoa maoni yao baada ya kusomwa kwa mara ya kwanza wiki iliyopita.
                                                
                     CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni: