mcharoman blogy fahar yako mtanzania
Si kila ombaomba aliye katika mitaa ya jijini Dar es Salaam au majiji na miji mingine nchini anatoka mkoani Dodoma.
Si kila ombaomba aliye katika mitaa ya jijini Dar es Salaam au majiji na miji mingine nchini anatoka mkoani Dodoma.
Hata hivyo, ipo dhana katika fikra za walio wengi
kuwa daima ombaomba hutokea mkoani Dodoma, jambo ambalo limedhihirika
kuwa halina ukweli, ingawa ni ukweli usiopingika kuwa wengi hutoka
katika baadhi ya vijiji vilivyo kwenye mwambao wa reli ya kati mkoani
humo.
Sababu za hali hiyo zinatajwa kuwa ni za
kimazingira ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa wananchi wa maaneo hayo
kuwa maskini, lakini nyingine inaelezwa ni hulka ya watu wengi katika
maeneo hayo kutopenda kufanya kazi ngumu hasa kilimo hivyo kuwa
ombaomba.
Makala haya hayalengi kuwazungumzia ombaomba, bali
maisha na changamoto za Hamisi Peter (44), mlemavu wa viungo ambaye
amekimbiwa na mkewe baada ya kupata ajali na kuthibitika kwamba atakuwa
akiishi maisha ya ulemavu.
Pia lengo si kuelezea tukio la Peter kukimbiwa na mkewe, bali maelezo yake kwamba hapendi na anachukia maisha ya kuombaomba.
“Mimi sipendi maisha haya ya kuombaomba, mwili
wangu unanilazimisha niishi hivi. Napenda nitoke katika maisha haya ya
aibu na manyanyaso makubwa. Nafsi yangu haifurahii maisha haya
yasiyokuwa na heshima, lakini nitafanya nini wakati watoto wawili
wananitazama mimi na mama yangu ambaye ni kikogwe pia ananitazama mimi?
Sina namna zaidi ya kuomba,” anasema Peter na kusisitiza:
“Ndiyo hivyo tena, ‘roho ipo radhi, lakini mwili
ni dhaifu’, sina budi kuishi kwa kuombaomba ili kunusuru maisha yangu na
watoto wawili waliotelekezewa na mke wangu.”
Anasema hawezi kuusahau mwaka 2011 kwani ndiyo uliobadili maisha yake na kuyaweka katika mitazamo mitatu.
“Nilijishughulisha na kazi halali za kuniingizia
kipato, lakini sasa ni ombaomba, pili; mwaka 2011 uliweka alama ya
mwisho wa uhusiano wa ndoa kati yangu na mke wangu, tatu; ni mwaka
uliogharimu viungo vyangu na sasa wananiita ‘Hamisi mlemavu,” anasema.
Anasema kuwa mwaka huo akiwa mkoani Morogoro
akifanya kazi ya kuuza nyama katika bucha lililomilikiwa na Hassan Idd,
siku moja alfajiri wakati wakienda machinjioni, gari walilotumia
lilipata ajali iliyogharimu maisha ya wenzake wawili, huku yeye
akiachiwa ulemavu.
Anasimulia kuwa baada ya ajali hiyo, alijikuta
akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro ambako kutokana na
hali yake ilivyokuwa, wataalamu katika hospitali hiyo walishauri
apelekwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), KCMC au Hospitali ya
Mkoa ya Dodoma (General Hospital) kwani huko kuna wataalamu wa mifupa
waliobobea.
Kutokana na ushauri huo, Peter anasema aliamua
kwenda Hospitali ya Dodoma kwa kuwa ni jirani na nyumbani kwao akiamini
ingekuwa rahisi kupata hata huduma nyingine. Hakika, akiwa hospitalini
hapo alihudumiwa ipasavyo akapona, ingawa amebaki akiwa mlemavu wa
viungo kutokana na nyoga na mguu wa kulia kuthibitika kuwa viliathirika
zaidi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni