promotion

Jumamosi, 18 Aprili 2015

UMEKAA NA KUJIULIZA NINI HASA SABABU YA AJALI HIZI ZILIZOTUANDAMA WIKI HII?

mcharoman blogy fahar yako mtanzania

Majanga yanazidi kughubika nchi na kuwamaliza Watanzania ambapo Kwa jana watu 39 walifariki dunia, huku wengine zaidi ya 100 wakijeruhiwa katika matukio tofauti ya kuangukiwa na kifusi na ajali ya gari lililotumbukia mtoni. 
 
Pia Watu 20 wanadaiwa kufariki papo hapo kwenye machimbo ya Kalole, wilayani Kahama na wengine kadhaa wanahofiwa miili yao ikiwa bado imefukiwa baada ya kuangukiwa na kifusi, mkoani Shinyanga wakati huko Rungwe watu 19, wamepoteza maisha katika ajali ya gari.
 
Katika tukio la Kahama wachimbaji wengine  zaidi ya 100, walijeruhiwa.
 
Akizungumza  jana, shuhuda wa tukio hilo, mfanyabiashara wa madini, Grace Makula, alisema mashimo matatu ya dhahabu yalidaiwa kuwapo na madini mengi na kusababisha wachimbaji hao kuvamia na kuanza kuchimba kwa vurugu hali iliyosababisha kuta kuporomoka na kuwafunika.
 
Makula alisema toka juzi mashimo hayo yalikuwa yametoa dhahabu nyingi kiasi cha wachimbaji kuuza na kupata hadi Sh. milioni 20, hali iliyochangia wengi zaidi kuvamia.
 
Alisema baadhi ya wafanyabishara toka jijini Mwanza walipopata taarifa ya mgodi huo kuwa na dhahabu kwa wingi, walifunga safari na kuwashawishi wachimbaji hao kuchimba kwa fujo na kusababisha madhara hayo.
 
“Hali hiyo ilisababisha wachimbaji kuchimba ili wapate dhahabu na kuuza kwa wafanyabiashara hao waliokuwa na pesa nyingi nje ya mashimo hayo yaliyopo kijijini Kalole,” alisema Makula.
 
Hata hivyo, alisema hadi jana saa 12:00 asubuhi, watu 20 walikuwa wametolewa katika mashimo hayo wakiwa wamepoteza maisha, huku idadi nyingine kubwa ikiwa chini ya mashimo hayo.
 
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, akizungumza , alisema jitihada za kutafuta miili ya watu wengine zinaendelea na taarifa rasmi zikitarajiwa kutolewa baadaye.
 
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alithibitisha kutokea kwa maafa hayo. Alisema jitihada za kuwatafuta watu wengine zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi na jeshi la polisi.
 
Huko Mbeya inaripotiwa kuwa watu 18  wamekufa papo hapo na mwingine akifariki baadaye ambapo wengine watatu wamejeruhiwa baada ya gari dogo la kusafirisha abiria aina ya Toyota Hiace kushindwa kukata kona kali eneo la Kiwira wilayani Rungwe, kupinduka na kutumbukia mtoni.
 
Ajali hiyo ilitokea jana katika eneo la Ilongobota, maarufu kwa jina la Uwanja wa Ndege, wakati basi hilo likitokea jijini Mbeya kwenda Tukuyu wilayani Rungwe.
 
Baadhi ya watu walioshudia ajali hiyo walisema kuwa gari hilo lenye namba za usajili T 290 ABU, lilikuwa kwenye mwendo mkali na kushindwa kukata kona na kujikuta likipaa na kutumbikia mtoni.
 
Shuhuda wa tukio hilo, Rashid Sumi, alisema kuwa baada ya gari hilo kutumbukia mtoni, akiwa pamoja na wananchi wengine waliwahi  eneo la tukio na kufanikiwa kuokoa watu wanne tu waliokuwa hai.
 
“Nilipofika hapa nilikuta maiti ya mtu mmoja tu ndiyo ilikuwa imetolewa, tulishirikiana kuwatoa, wengi walikuwa wamekufa na tulitoa watu wanne tu waliokuwa hai, lakini wakiwa wamejeruhiwa vibaya,” alisema Sumi.
 
Alisema kuwa majeruhi pamoja na maiti zote zilichukuliwa kukimbizwa hospitalini, lakini wakiwa njiani majeruhi mmoja pia alipoteza maisha.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kudai kuwa chanzo chake ni mwendokasi wa gari hilo.
 
Kamanda Msangi, alisema gari hilo likiwa kwenye mwendo kasi, dereva alishindwa kulimudu, hali iliyomfanya ashindwe kukata kona na kujikuta gari likienda kutumbukia kwenye daraja la mto Kiwira.
 
Alisema kuwa eneo hilo la Ilongobota ni hatari kwa kuwa kuna mteremko mkali na kona nyingi hivyo madereva wanapofika kwenye eneo hilo wanapaswa kuwa makini zaidi.
 
“Ajali hii imetokea majira ya saa 3:00 asubuhi wakati dereva wa gari hili akiwa kwenye mwendo kasi uliosababisha ashindwe kulimudu na kujikuta akitumbukia darajani,” alisema Kamanda Msangi na kuongeza
 
“Katika ajali hii watu 17 walikufa pale pale na wengine wanne walijeruhiwa, lakini wakati wakikimbizwa hospitalini, mmoja alipoteza maisha na kufanya idadi ya watu waliokufa kufikia 18,” alisema Kamanda Msangi.
 
Kamanda Msangi alitoa wito kwa madereva kuwa makini wawapo barabarani kwa kuzingatia sheria na kutoendesha magari kwa mwendo kasi kuliko uwezo wao ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
 
Hata hivyo, alisema gari hilo lilisajiliwa kwa ajili ya kufanya safari katika Jiji la Mbeya kama daladala, lakini dereva kwa tamaa zake aliamua kusafirisha abiria kwenda Tukuyu.
 
Alisema kuwa uamuzi wa dereva huyo kwenda sehemu asiyotakiwa ilitokana na madereva wa magari yanayosafirisha abiria kutoka Mbeya kwenda Kyela kupitia Tukuyu kugoma na hivyo kufanya hali ya usafiri katika barabara hiyo kuwa tete.
 
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Aminiel Ngumo, alikiri kupokea miili ya watu 18 ambayo kati yake 17 imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Rungwe ya Makandana na moja katika Hospitali ya Misheni ya Igogwe.
 
Alisema majeruhi wengine watatu wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Igogwe na kwamba hali zao zinaendelea vizuri.
 
CHADEMA, CUF  VYAZUNGUMZIA AJALI
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, amemtaka Rais Jakaya Kikwete aeleze hatua ilizochukua serikali kukomesha matukio ya ajali zinazotokea kila siku nchini.
 
Aidha, amemtaka Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, aiweke hadharani ripoti ya uchunguzi na utangulizi wake kuhusu kujirudia kwa ajali hapa nchini.
 
Akizungumza na wanahabari jana jijini Dar es Salaam, Mnyika alisema kuwa,  ikiwa serikali haitafanya hivyo, Chadema itaeleza hatua gani zinapaswa kuchukuliwa.
 
Alisema nchi inapaswa kujiuliza itatoa pole mpaka lini kwa ajali zinazoendelea kutokea na kupoteza Watanzania wengi.
Alisema serikali imekuwa na ukimya kuhusu ajali hizo mara zote imekuwa ikitoa pole ambazo sio suluhisho wa kumaliza changamoto zilizopo.
 
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama hicho, limetaja sababu za ajali nyingi ni miundombinu, magari mabovu na madereva kwenda mwendo kasi, mafunzo hafifu ya salama barabarani kwa madereva wa malori na mabasi ya abiria.
 
Alisema vitendo vya rushwa katika utoaji wa leseni na usimamizi wa usalama barabarani ni moja ya sababu za ajali hizo.
Alisema baraza hilo linaitaka serikali kufanya utafiti wa kina kuhusu sababu za ongezeko la ajali hizo na kuweka utaratibu madhubuti wa kusimamia usalama barabarani.
 
Mapema wiki hii, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama barabarani nchini, Mohamed Mpinga, alisema watu 103 wamepoteza maisha na wengine 138 kujeruhiwa kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Machi 11 hadi Aprili 12, mwaka huu, kutokana na ajali za barabarani.
 
Alisema kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi sasa ajali zilizotokea ni nane huku vifo vikiwa ni 103 na majeruhi 138.
Mpinga alisema kwa kipindi cha miezi mitatu Januari hadi Machi kumetokea vifo vya watu 866 na majeruhi 2,370 kutokana na ajali hizo.
 

Hakuna maoni: