promotion

Jumatatu, 13 Aprili 2015

NJIA BORA YA KUISHI NA MARAFIKI WA MWENZI WAKO

mcharoman blogy fahar yako mtanzania





Kwa lugha nyepesi namaanisha kama wewe ni mwanaume, unawezaje kuishi na marafiki wa kike wa mwenzi wako na kama wewe ni mwanamke, unawezaje kuishi na marafiki wa kiume wa mwenzi wako?
Wiki iliyopita, tulijadili kwamba jambo la kwanza ni kujiheshimu na la pili ni kujiwekea mipaka. Leo tunaendelea na njia nyingine za namna ya kuishi vizuri na marafiki wa mwenzi wako.

3. EPUKA KUKUTANA NAO MKIWA PEKE YENU
Mathalani wewe ni mwanamke na kuna rafiki wa kiume wa mwenzi wako anakupigia simu na kukushawishi ukutane naye sehemu fulani, tena mkiwa wawili tu huku akikusisitiza kwamba mwenzi wako hapaswi kujua, hiyo ni dalili kwamba ana nia mbaya na wewe.

Kama kweli unampenda mwenzi wako na haupo tayari kumpoteza, unapaswa kumueleza kuhusu suala hilo na kwa pamoja mjue namna ya kukomesha tabia hiyo.
Endapo ukikubali kuanza kuwa unakutana naye katika mazingira yaliyojaa utata, utakuwa unahatarisha uhusiano wako.
Kwa mfano siku ikatokea ghafla mwenzi wako akakukuta ukiwa na rafiki yake, katika mazingira yaliyojaa utata, tena mwenyewe akiwa hana taarifa yoyote juu ya kukutana kwenu unategemea utakuelewa vipi?

4. KUWA NA MSIMAMO
Kuna usemi ambao siku hizi umezoeleka kwamba kwa mwanamke kutongozwa ni suala ambalo haliepukiki. Wanaume wengi wana hulka ya kupenda kutongoza bila kujali anayemtongoza ni nani.
 Hata kama anajua kabisa huyu ni mke wa rafiki yake, atajaribu kumtongoza na kumchombeza kwa maneno ya kimapenzi.
Endapo mwanamke atakosa msimamo, ni dhahiri atakubali kwa kuamini kwamba anapendwa sana na mwisho itakuwa ni kumsaliti mwenzi wake ambaye ndiye aliyemfanya akafahamiana na huyo anayemtongoza. Huu ni ulimbukeni wa hali ya juu kwa sababu unapotongozwa hulazimishwi kukubali.

Mwanamke mwenye msimamo, anaweza kukabiliana vyema na hila za wanaume, wakiwemo marafiki wa karibu wa mume wake bila kusababisha usaliti wa aina yoyote. Kama kweli unampenda, kuwa na msimamo na usiwe mwepesi wa kukubali kila unapotongozwa.

5. DUMISHA UAMINIFU
Njia kubwa kuliko zote ambayo inaweza kuufanya uhusiano wako na mwenzi wako kuwa salama muda wote, ni kudumisha uaminifu katika mapenzi yenu, bila kujali kama mwenzi wako yuko na wewe au yupo mbali.
Jiwekee nadhiri kwamba utampenda, kumlinda na kumheshimu siku zote na kwamba huwezi kumsaliti hata iweje.
 Ifanyie kazi nadhiri yako na hakika, hakuna kitakachokuyumbisha.
Kwa leo tuishie hapa, kwa mada nyingine tukutane wiki ijayo.
Kwa maoni, ushauri, nicheki kwa namba za hapo juu.

Hakuna maoni: