mcharoman blogy fahar yako mtanzania
Kudra Janja akiwa na majeraha mwili mzima baada ya kulipuliwa na mumewe kwa petrol.
|
Mwanamke mmoja, Kudra Janja mkazi wa Kijiji cha Bwai, wilayani Butiama mkoani Mara amelipuliwa kwa petroli na mumewe, Simon Otieno kwa kile kilichodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.Katika tukio hilo pia mtoto aliyejulikana kwa jina la Tatu Simon (1) alifariki dunia muda mfupi baada ya kuungua kwa moto katika unyama huo uliofanywa na baba yake mzazi.
Habari kutoka katika kijiji hicho zinasema kwamba mume wa mama huyo, Simon aliamua kuwamiminia petroli mke na mtoto wake kupitia dirishani kisha kulipua kwa moto chumba ambacho wawili hao walikuwa wamelala Machi 31, mwaka huu.
Kudra ameungua vibaya mwili mzima na alilazwa katika Hospitali ya Mara na baadaye kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza wakati mtoto wake alikutwa ndani ya nyumba hiyo akiwa ameungua vibaya na baadaye kufariki dunia.
Mama mdogo wa Kudra aliyejitambulisha kwa jina la Bahati Magesa aliliambia gazeti hili kuwa tukio hilo lilitokea nyumbani kwa mjomba wao saa 10 usiku.“Kisa cha tukio hili ni ugomvi wa siku nyingi unaotokana na wivu wa mapenzi kwa watu hawa ambao wameishi pamoja kwa muda wa mwaka mmoja tu,” alisema Bahati.
“Otieno alikuwa akimtuhumu mke wake kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na watu wengine lakini baadaye ugomvi huo uliisha na wakawa wanaendelea na maisha yao vizuri.“Baada ya tukio hili Kudra ambaye ni mtoto wa dada yangu aliniambia kuwa mumewe aliingia ndani akiwa na dumu la petroli na alipomuuliza la nini alimuambia alale, halimhusu.
“Baadaye alimwaga mafuta dirishani akachukua kibiriti na kutoka nje akawasha na kuacha mlipuko mkubwa na yeye kutokomea kusikojulikana.“Baada ya moto kulipuka, Kudra alipiga yowe ndipo mjomba wake, Obadia Janja alikimbilia na kwenda kumuokoa na akamtoa nje na mtoto wake wakati moto unawaka kwa kasi.
“Mama alikuwa ameungua mwili mzima na mtoto aliungua vibaya sana na baada ya muda mfupi aliaga dunia,” alisema Bahati.Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Philip Kalangi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Tumeanza kumtafuta Simon Otieno ambaye amefanya tukio la kinyama na linapaswa kulaaniwa na kila mmoja. Ninaiomba jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi,” alisema Kamanda Kalangi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni