mcharoman blogy fahar yako mtanzania
Hatimaye mwalimu wa chekechea, Mollen Calleb, aliyesimama mahakamani kwa kujifanya mzazi wa mtoto wa miaka miwili aliyejeruhiwa kwa kupigwa na mlezi wa shule ya chekechea ya Nelca Day, amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kuidanganya mahakama.
Kaimu Kamanda, Kamishna Msaidizi wa Polisi jijini Mwanza (ACP), Japhet Lusingu. |
Ni mwalimu aliyejifanya mzazi wa mwanafunzi .
Katika tukio hilo, mwalimu huyo aliidanganya mahakama na kusababisha kesi hiyo ya kujeruhi kufutwa bila mlalamikaji kuwapo mahakamani.
Machi 27, mwaka huu, katika Mahakama ya Mwanzo Ilemela, jijini Mwanza, ilifuta kesi ya kujeruhiwa mwanafunzi, inayomkabili mlezi wa shule ya chekechea ya Nelca Day Care, Siwema Bujota, anayedaiwa kumpiga mtoto huyo na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili.
Bujota aliyekuwa na dhamana ya kulea watoto shuleni hapo, alimjeruhi mwanafunzi wa miaka miwili (jina limehifadhiwa), kwa kumchapa viboko maeneo mbalimbali ya mwili wake kwa madai kuwa alijisaidia haja kubwa shuleni.
Baada ya kesi hiyo kufikishwa mahakamani, mwalimu wa shule hiyo, Calleb alikwenda mahakamani na kujitambulisha kwamba yeye ndiye mlalamikaji wa kesi hiyo na kuiomba mahakama kuifuta kwa madai kuwa hakuwa na nia ya kuendelea na mashitaka na kwamba watamalizana nje ya mahakama.Kutokana na maelezo hayo, hakimu aliyetambulika kwa jina moja la Misana wa mahakama hiyo, alifuta kesi hiyo bila kujua kama huyo aliyesimama mahakamani si mlalamikaji halali.
Mlalamkaji katika kesi hiyo alikuwa Sabrina Hamis, ambaye kabla ya kesi kuanza kusikilizwa alikwenda hospitali kwa matibabu ya mtoto huyo, ambaye hali yake ilibadilika ghafla.
Kufuatia tukio hilo, Hamis alikwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi cha Kilumba, kulalamikia kesi yake kufutwa kinyemela.
Jeshi la polisi mkoani Mwanza lilianza kuwasaka watuhumiwa wote wawili akiwemo mshtakiwa na mwalimu aliyejifanya mlalamikaji.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, Kaimu Kamanda, Kamishina Msaidizi wa Polisi jijini Mwanza (ACP), Japhet Lusingu, alisema kuwa Aprili 13, mwaka huu, watuhumiwa hao walikamatwa.
Alisema Aprili 14, mwaka huu walifikishwa mahakamani na kupata taarifa kwamba mwalimu huyo amefungwa miezi sita kwa kuidanganya mahakama.
NIPASHE ilizungumza na mlalamikaji ambaye alisema mwalimu huyo amehukumiwa kwenda jela miezi sita kwa kuidanganya mahakama. Aidha, alisema mtuhumiwa alipelekwa rumande hadi Aprili 23, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
CHANZO: NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni