promotion

Jumapili, 29 Machi 2015

UCHAWI WAFUMULIWA SOKONI




 
WE acha tu! Sangoma mmoja aliyejulikana kwa jina la Mohamed Chimwaganje (44), amezua kizaazaa katika Soko la Kapera lililopo Mwembechai jijini Dar kufuatia kufumua vitu chini ya ardhi vinavyodhaniwa ni vya ushirikina,  Risasi Jumamosi linakujuza.

Sangoma Mohamed Chimwaganje akishika hirizi aliyoitoa katika Soko la Kapera lililopo Mwembechai jijini Dar.
Tukio hilo la aina yake lilijiri asubuhi ya Machi 25, mwaka huu katika soko hilo ambapo awali taarifa zilimfikia sangoma huyo kwamba, baadhi ya  wafanyabiashara wa soko hilo wamekuwa wakiibiwa pesa zao kwa njia ya maajabu  .
MFANYABIASHARA AZUNGUMZA
Akizungumza na Risasi Jumamosi, mmoja wa mashuhuda sokoni hapo alisema kuwa, ilifika wakati wafanyabiashara hao walikuwa hawaingizi faida wakiwa sokoni hapo na wanaweza wakauza lakini kwenye mahesabu jioni, pesa kibao zimepotea, hivyo kusababisha wengi kuacha biashara baada ya kufilisika.
“Lakini cha kushangaza ni kwamba, baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo wamekuwa wakiuza sana vitu visivyokuwa na ubora na vile vyenye ubora kuachwa na wateja ambapo mwishowe huharibika na kutupwa.“Basi, kutokana na hali hiyo tukaamua kumwomba huyo mtaalamu ‘sangoma’ aje afanye mambo yake maana tunamwamini kwa sababu  ameshamponya uchizi mtu mmoja wa hapa mtaani,” alisema mfanyabiashara huyo akikataa kutaja jina lake gazetini.

Moja ya hirizi iliyotolewa katika soko hilo.
UMATI WAMZUNGUKA SANGOMA
Waandishi wetu wakiwa eneo la tukio walishuhudia umati sokoni hapo ukiwa umemzunguka sangoma huyo ambapo alipandisha mzuka wake na kusema kuna wafanyabiashara wanne ambao wamechimbia hirizi sokoni hapo ili kukusanya fedha za wenzao kwa njia ya chuma ulete.
Sangoma huyo aliendelea kusema kuwa, kazi ya hirizi hiyo ni kutoa kafara ya kuua mtu yeyote anayepita sokoni hapo kila baada ya miezi sita lakini pia kuna chungu ambacho kimekuwa kikikusanya fedha hizo, maneno yaliyowafanya wateja sokoni hapo wapigwe butwaa.
SANGOMA AANZA KUFUMUA
Baada ya kusema hayo, Risasi Jumamosi lilimshuhudia sangoma huyo akianza kuchimba ardhi katikati ya soko hilo na chini yake kwenye shimo alitoa hirizi hiyo iliyozungushwa ushanga.Sangoma aliimwagia maji maalum hirizi hiyo. Alisema maji hayo ni moja ya dawa zake za kupoza makali ya hirizi na kisha akaiteketeza kwa moto.

...Sangoma akiichoma hirizi hiyo.
USHIRIKINA MWINGINE
Ukiacha mbali hirizi, vitu vingine alivyoviibua sangoma huyo ni meno ya samaki hatari baharini aitwaye  papa, chupa kadhaa za pafyumu zilizochanganywa na maji ya maiti za watu na paka ambao hutumika pia kuchukua bidhaa kimazingara sokoni hapo.

MZUKA WA SANGOMA WAPOA, AONGEA NA RISASI JUMAMOSI
Risasi Jumamosi lilisubiri mzuka wa mganga huyo utulie ndipo likazungumza naye ambapo katika maelezo yake alisema hirizi aliyoiibua ardhini  ilitengenezwa kwa kutumia sehemu za siri za wanawake ambao hawajazaa.“Inavyotokea ni kwamba, maiti za wanawake hukatwa kwa siri wakati wa kuoshwa na watu wa mochwari kabla ya kuuzwa kwa watu wanaozitumia kishirikina,” alisema sangoma huyo.

Wateja waliokuja kununua bidhaa sokoni hapo wakishuhudia tukio hilo.
NI MEZA KWA MEZA
Sangoma alisisitiza kuwa, oparesheni hiyo itakuwa meza hadi meza pamoja na kuwaumbua wale wote wenye tabia za kishirikina na hatamuogopa mtu wala yeye haogopi kufa kwa vile mizimu yake imemtuma kuwasaidia wote wenye matatizo kulingana na anavyoelekezwa.

Imeandaliwa na: Deogratius Mongela, Chande Abdallah na Mayasa Mariwata

Hakuna maoni: