promotion

Jumanne, 31 Machi 2015

MAMA ADAI KUJIFUNGUA MTOTO WA KIUME, APEWA WA KIKE TENA MAITI

mcharoman blogy fahar yako mtanzania

SKENDO mpya imeikumba Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kufuatia mwanamke mmoja, Rukia Fikiri (pichani) kudai kujifungua mtoto wa kiume kisha baadaye kukabidhiwa mtoto wa kike akiwa amefariki dunia, .Tukio hilo la kushangaza lilijiri Machi 25, mwaka huu katika wodi ya wazazi ya hospitali hiyo.Rukia Fikiri(kulia) akiwa na ndugu zake wakiwa wamebeba maiti ya mtoto wanaodai kubadilishiwa na manesi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
MSIKIE MWENYEWE
Akizungumza na Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita hospitalini hapo, Rukia alisema alijifungua mtoto wa kiume mwenye afya njema saa 6 usiku wa Machi 24, mwaka huu na kwamba baada ya kujifungua alionyeshwa kisha aliondolewa leba na kupelekwa Wodi ya Wazazi 7 B.
“Lakini kutokana na uchungu wa uzazi kule wodini nilipitiwa na usingizi. Nilipokuja kuamka, manesi waliokuwa wakinihudumia na mtoto wangu waliniambia mtoto amefariki dunia.“Niliumia sana, nilitoa taarifa kwa ndugu zangu akiwemo mume wangu ambapo walifika hapa tukakabidhiwa maiti huku manesi wakisema wameifunga kwa nguo, wakasema tukaifungulie nyumbani,” alisema Rukia, akaongeza:
“Tulienda nyumbani kwa wakwe zangu eneo la Chamwino. Tulipofungua maiti kwa lengo la kuiosha ili tukaisitiri, tulishangaa kuona ni ya mtoto wa kike badala ya wa kiume.”“Haraka sana tukagundua manesi walitubadilishia. Tulikaa kikao cha dharura cha familia, tukakubaliana tuirudishe maiti hapa. Mimi ninamtaka mtoto wangu wa kiume awe hai au amekufa,” alisema mwanamke huyo huku akiangua kilio kwa uchungu.
Rukia Fikiri anayedai kubadilishiwa mtoto huyo.
MUME NAYE AZUNGUMZA
Mume wa Rukia, Hamidu Fikiri naye alipata fursa, akazungumza na Uwazi na kusema:
“Kitendo walichofanya wale manesi ni cha kushangaza sana, kama nisipopewa mwanangu tutaelewana vibaya, mimi nimeshakwenda polisi.”
Mama mzazi wa Hamidu, Mariam Seif ambaye ni bibi wa mtoto alisema kitendo cha mjukuu wake ‘kuibwa’ wodini kimemsikitisha na hawezi kuzika mtoto wa mtu mwingine.“Tulipomrudisha mtoto hapa hospitalini, manesi walikuwa wakitupiana mpira, wale wa wodi 7 B wanasema tatizo liko leba, wa leba wanasema kinyume chake,” alisema bibi huyo.Taarifa zinasema, polisi waliamuru mwili wa mtoto huyo uhifadhiwe hospitalini hapo huku uchunguzi ukiendelea.
Uwazi lilipompigia simu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Rita Lyamuya hakupatikana ofisini kwake na hata alipotafutwa kwa njia ya simu yake ya mkononi, iliita bila kupokelewa.
MASWALI MAGUMU
Ndani ya cheti cha mzazi kulazwa na kuruhusiwa kuna maandishi ya msingi wa uzazi yanayosomeka: Complete Abortion ‘CA’  (mimba kuharibika) ikimaanisha ndicho kiini cha mzazi huyo kufikishwa hospitalini hapo.
Uwazi lilijiuliza kwa nini cheti hicho kiandikwe hivyo wakati mzazi anadai alijifungua salama tena leba?
Daktari mmoja wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (jina lipo), alipoulizwa na gazeti hili kuhusu hali hiyo, alisema: “Complete Abortion ni mimba imetoka kabla ya muda wa kujifungua. Lakini kama huyo mama aliingizwa leba ina maana alijifungua, wasingeandika Complete Abortion, wangeandika SB, kwamba amejifungua salama.
“Mwanamke wa CA hawezi kupelekwa leba. Kutakuwa na tatizo katika uandishi wa hicho cheti. Kwani mtoto mwenyewe alikuaje hata kama alifariki dunia?”Uwazi: “Mwili wa mtoto upo kamili, ila ni marehemu tu.”
Dokta: “Sasa CA mtoto hawezi kuwa kamili. Nadhani hapo katika uandishi wa cheti pana tatizo.”
Gazeti ili linaendelea na uchunguzi.