promotion

Jumamosi, 21 Machi 2015

KUMBE UTORO SIO SHULENI AU VYUONI HATA BUNGENI PIA UPO (Wabunge 200 watoro)

                      mcharoman blogy fahar yako mtanzania



Hali ya utoro kwenye vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano sasa imekithiri baada ya ofisi ya chombo hicho cha kutunga sheria kusema kina taarifa za wabunge 15 tu walioomba ruhusa kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Bunge hilo, linalotakiwa kuwa na wabunge 357, lilishindwa kupitisha miswada mitatu kutokana na upitishwaji wake kuhitaji theluthi mbili ya wabunge wa kila upande wa Muungano.
Jana, wakati wa mjadala wa muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa ambao uliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), Jenister Mhagama kulikuwa na idadi ya wabunge 81 tu bungeni, jambo linalomaanisha kuwa takriban wabunge 250 hawakuwamo ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria.
Hali ilikuwa mbaya zaidi juzi. Wakati kikao cha Bunge kikianza kujadili Muswada wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi, kulikuwa na wabunge 29 tu ukumbini, hali inayomaanisha kuwa zaidi ya wabunge 320 hawakumo ndani kujadili suala hilo nyeti.
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge,  John Joel aliiambia Mwananchi jana kuwa ni wabunge 15 tu ndiyo ambao wana ruhusu ya Spika ya kutoshiriki kwenye vikao vinavyoendelea na kwamba wengine wote wanapaswa kuwa bungeni.
“Wabunge 15 tu ndiyo wenye ruhusa, wengine wapo lakini wanaingia na kutoka bungeni. Kutokuwepo kwao kunaathiri sana wakati wa kupitisha miswada kutokana na kutotimia kwa akidi.”
Idadi ya wabunge walio na ruhusa ni ndogo sana kulinganisha na viti vingi vinavyokuwa vitupu wakati wa mijadala mbalimbali kwenye vikao vya Mkutano wa 19 vinavyoendelea mjini hapa, jambo ambalo ofisi ya Bunge imeleza kuwa inathiri shughuli mbalimbali za Bunge zinazotakiwa kufanyika. Kwa mpangilio wa viti bungeni, kawaida safu tatu tu za eneo moja huweza kuwa na viti zaidi ya 15.
Wawakilishi hao wa wananchi wanalipwa Sh300,000 kwa siku, ikiwa ni fedha za posho ya kujikimu na vikao, kiwango ambacho kwa kuzidisha kwa idadi ya wabunge 357 inafanya jumla ya Sh107.1 milioni kutumika kwa siku moja.
Tangu kuanza kwa vikao vya Mkutano wa 19 wa Bunge  Machi 17 mwaka huu hadi jana mchana, idadi ya wabunge imekuwa ndogo ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge uliokuwa na mahudhurio makubwa kutokana na kujadili sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Katika mkutano wa 18 ulioisha Februari mwaka huu wabunge wengi walikuwa wakichangia hoja, walijikita katika kuzungumzia matatizo ya majimbo yao na kuacha mjadala uliokuwa mezani, jambo ambalo lilimfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwataka wajikite kwenye hoja za msingi na si kuzungumzia masuala ya majimbo yao.
Katika mkutano wa 19 unaoendelea hivi sasa wabunge wamekuwa ni wachache, hali ambayo hulalamikiwa na baadhi ya wabunge hasa ukifika muda wa kupitisha miswada mbalimbali.
Jana, kaimu kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema kuwa utoro wa wabunge unakwamisha mambo mengi ya msingi bungeni, huku akibainisha kuwa miswada haiwezi kupitishwa huku kukiwa na idadi ndogo ya wabunge na kwamba kufanya hivyo ni kukiuka kanuni.