mcharoman blogy fahar yako mtanzania
Wakati msako wa kukamata wapiga ramli chonganishi ukiendelea nchi nzima hasa katika mikoa ya kanda ziwa, jeshi la polisi nchini limepewa onyo kali kutoka kwa waganga wa jadi juu ya vifaa vinavyokamatwa wakati wa msako huo.
Jeshi hilo limepewa tahadhari ya kukumbana na hatari yoyote wakati wa baadaye, ikiwa litaendelea kukamata vifaa hivyo vikiwemo vibuyu, vitambaa vyeupe na vyeusi, ngao, mikuki, pamoja na shanga huku likitakiwa kurejesha mara moja baadhi ya vifaa hivyo ambavyo vimekamtwa.
Tahadhari hiyo ilitolewa jana na Katibu Mwenezi wa chama cha waganga wa Tiba Asili Tanzania (CHAWATIATA) Bw. Steven Sebastian kutoka Mkoani Mwanza, wakati akiongea katika Mkutano wa waganga wa jadi Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu uliofanyika katika ukumbi wa CCM Bariadi.
Katibu huyo akiongea mbele ya Mkuu wa polisi Mkoani Simiyu Charles Mkumbo alisema kuwa kitendo kinachofanyana jeshi hilo cha kukamata vifaa hivyo, ni kitendo cha hatari kwani kinaweza kusababisha hali ya migogoro mikubwa kati ya jeshi la polisi na jamii.
Sebastian alieleza kuwa vibuyu, vitambaa vyeupe, na vyekundu, shanga, ngao, pamoja na mikuki, ni vifaa ambavyo waganga hao walirishwa na wazee wa zamani ambao alieleza kuwa vifaa hivyo walivitumia katika kutafuta uhuru.
Aidha alisema kuwa endapo zoezi hilo litaendelea bila ya kusitishwa upo uwezekano mkubwa na wazee hao wa zamani kukasirika kwa kiasi kikubwa kutokana na kugusa vifaa vyao ambavyo walivirisisha kwa watoto wao ambao ni waganga wa jadi wanatuhumiwa kupiga ramli chonganishi.
“ Nitoe tahadhari mbele yako Mkuu wa polisi msako huu unaoendelea umelenga kusambaratisha jadi wakati ndizo zilizotumika kuleta uhuru…vifaa hivi vinavyokamatwa virejeshwe mara moja…wazee hawa wakikasirika hakuna hatakaye baki ndani ya jeshi la polisi..msitake kugombana na mila..gomba na wanapiga ramli chonganishi..lakini chonde chonde rejesheni vibuyu vyetu haraka” Alisema Kiongozi huyo
Alieleza kuwa viongozi wa zamani wa makabila mbalimbali ( machifu) walikuwa wanatumia vifaa hivyo kufanyia kazi mbalimbali ambazo alisema kuwa zilikuwa zinatumika vizuri na siyo kuwa zinatumika katika kuua watu kama inavyodhaniwa.
Alisema kuwa wazee hao wanaweza kukasirika wakati wowote kuanzia hivi sasa ikiwa vibuyu vyao vitaendelea kukamatwa, sambamba na vingine vitashindwa kurejeshwa kwa wamiliki wao waliowaachia.
Alilitaka jeshi hilo kuacha mara moja kupeleka chuki za moja kwa moja kwa waganga wa jadi ambao wanatumia vifaa hivyo kwa nia njema, na badala yake chuki hizo zielekezwe kwa wanaopiga ramli chonganishi.
Aidha Katibu huyo alisema kuwa kwa watuhumiwa wanatakaobainika ndiyo chanzo cha kuuawa au kukatwa kwa viungo vya watu wenye ulemavu wa Ngozi (Albino), alitaka adhabu yao iwe kunyongwa hadharani.
Akiongelea hoja hiyo Mkuu huyo wa polisi Mkoani Simiyu alieleza kuwa siyo kweli kuwa waganga wa jadi wanaonewa au kusingiziwa kuwa hawapigi ramli chonganishi bali katika uchunguzi wao wamebainika kuwa ndiyo chanzo kikuu.
Aliwataka waganga ho kuacha mara moja vitendo hivyo, huku akiwataka kila mmoja kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja anapatiwa leseni au kujiandikisha kwa viongozi wao wa vijiji au mtaa ili kuweza kukwepa msako mkali utakaoanza baada ya mwezi mmoja.
Hata hivyo waganga hao walifanya uchaguzi katika Mkutano huo ambapo walimchagua Mayunga Kidoyai kuwa Mwenyekiti, Shinyanga Isamila Makamu Mwenyekiti, Njile Kasula Katibu, pamoja na John Kunini ambaye alichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi.