Philip Hammond waziri wa mambo ya nje wa Uingereza |
Mazungumzo kuhusu mpango tata wa Iran wa nyuklia yameendelea nchini Uswisi, kwa kuwasili mawaziri wa mambo ya nje kutoka mataifa sita yenye nguvu duniani.
Kiongozi wa mazungumzo wa Iran Abbas Araqchi amesema makubaliano yanawezekana-- lakini mazungumzo yakjo katika hatua ngumu na bado kuna mambo ya kutatua.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Philip Hammond pia amesema anaamini makubaliano yatafikiwa lakini yatatakiwa kuhakikisha Iran haipati uwezo wa kutengeneza bomu la nyuklia.
Mazungumzo mjini Lausanne yataendelea leo kabla ya siku ya mwisho ya kufikiwa mkataba wa muundo wa mazungumzo hayo hayo kesho, Jumanne.
Maafisa wa Marekani wanasema bado kuna kutokubaliana kuhusu namna ya kuiondolea Iran vikwazo, na namna itakavyokuwa huru kuendeleza utafiti wa nyuklia."tupo hapa kwa sababu tunaamini mkataba unaweza kufanyika. Ni kwa masilahi ya kila mmoja kuona mkataba unafanyika. Lakini unatakiwa kuwa mkataba ambao unaizuia Iran kupata uwezo wa kutengeneza bomu. Hakutakuwa na maelewano kuhusu hilo. Kwa hiyo iwapo tutafanikisha hili katika saa chahche zijazo, Iran itatakiwa kupata ahueni na kuchukua maamuzi magumu kuhakikisha kwamba mambo yanayoleta ugumu katika suala hilo yanatatuliwa. Ni matumaini makubwa kwamba tutafanikiwa katika saa zijazo."Amesema Bwana Hammond.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, ametoa tathmini yenye kutia matumaini kuhusu mazungumzo hayo lakini ameonya kuwa yanaweza kuleta mvutano. "Kwa sasa vizuri sana, lakini, lakini hili linaweza kubadilika kwa sababu ya tofauti ambazo hazijaweza kupatiwa ufumbuzi kwa upande wetu lakini tunakaribia karibu zaidi katika saa chache zijazo. Siwezi kutupilia mbali na hili daima imekuwa kawaida katika mazungumzo kama haya ambako maslahi ni makubwa na katika hali ambayo tunahisi tunawajibika si tu kwa upande wetu lakini kwa wote ambao hawapo katika mazungumzo- Siwezi kutupilia mbali kwamba kutakuwa na mgogoro zaidi katika mazungumzo haya."