Kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda. |
Kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, zimeendelea huku upande wa mashtaka ukiwasilisha mkanda wa video unaodaiwa kuonyesha uhalisia wa tukio zima la kesi hiyo ambayo anatuhumiwa kutoa maneno ya uchochezi.
Mkanda huyo uliletwa mahakamani mbele ya Hakimu mkazi Mkoa wa Morogoro, Mary Moyo, na kuonyeshwa na shahidi wa tano wa kesi hiyo ambaye ni askari kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi Kitengo Maalumu cha Uchunguzi wa picha mwenye namba E2587 D/SSGT Aristides.
Shahidi hiyo alieleza vigezo alivyovitumia kutambua uhalisia wa video hiyo iliyochukuliwa Agosti 10, 2013.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Benard Kongola, alieleza mahakamani kuwa video aliichunguza na kugundua kuwa ilichukuliwa katika eneo la tukio kupitia kamera ndogo aina ya JVC na kwamba baada ya kuichunguza aliandika hati na taarifa iliyoeleza vigezo alivyovitumia katika uchunguzi huo na yale aliyoyaona na kuyasikia katika video hiyo ambayo aliitoa mahakamani kama kielelezo.
Video hiyo ilionyesha tukio zima pamoja na maneno aliyoyatoa Sheikh Ponda ambayo yanadaiwa kuwa yalikuwa ya uchochezi na yaliyoingilia imani ya dini zingine.
Awali, aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alikuwa shahidi wa nne kutoa ushahidi jana asubuhi na kueleza kuwa baada ya kupata taarifa za kutafutwa kwa Sheikh Ponda kufuatia tuhuma mbalimbali zilizomkabili, aliandaa askari kwa ajili ya kumkamata baada ya kufika mkoani Morogoro.
Shahidi huyo alidai kuwa taarifa hizo za kiinterejensia zilimuhusisha Sheikh Ponda na tuhuma za kuwamwagia tindikali wasichana wawili, raia wa Uingereza mjini Unguja na tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi jijini Dar es Salaam na kwamba tuhuma hizo alizipata wakati akiwa kwenye adhabu ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja na kupewa sharti la kutofanya kosa lolote katika kipindi hicho.
Kwa Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Juma Nasoro ulimuuliza maswali shahidi huyo, hata hivyo baadhi ya watu waliokuwapo mahakamani hapo walishindwa kuzuia vicheko vyao kutokana na aina ya maswali yaliyokuwa yakiulizwa pamoja na majibu yaliyokuwa yakitolewa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni