Ufaulu katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne umeongezeka kwa asilimia 10, chini kidogo ya viwango vya Matokeo Makubwa Sasa (BRN), lakini shule za Serikali za vipaji maalumu, kongwe na za seminari zimeendelea kuporomoka.
Katika matokeo hayo, Shule ya Sekondari ya Kaizirege ya mkoani Kagera, iliyoanzishwa mwaka 2010, ndiyo imekuwa kinara ikiwa ni mwendelezo wa mafanikio baada ya mwaka jana kushika nafasi hiyo lakini kwa upande wa shule zenye watahiniwa chini ya 40. Shule iliyoshika mkia ni Manolo iliyopo Tanga, mkoa ambao umetoa shule tano miongoni mwa shule zilizoshika nafasi 10 za mwisho.
Matokeo hayo ni ya kwanza tangu kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa upangaji wa Wastani kwa Kutumia Pointi (GPA) ambao unaonyesha shule zote 10 za kwanza ni za binafsi.
Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk Charles Msonde alisema waliofaulu mtihani huo ni wanafunzi 196,805 sawa na asilimia 68.33 ya watahiniwa 288,247 waliofanya mtihani huo, ikilinganishwa na 235,227, sawa na asilimia 58.25 ya waliofaulu mwaka 2013.
Dk Msonde alisema wavulana waliofaulu ni 106,960 sawa na asilimia 69.85 na wasichana ni 89,845 sawa na asilimia 66.61.
Kwa mujibu wa maelekezo ya BRN, ufaulu wa upande wa sekta ya elimu, ambayo ilipangiwa malengo tisa, ulipaswa uwe asilimia 70.
Hata hivyo, pamoja na kuwa chini kidogo ( asilimia 1.7) kufikia wastani wa ufaulu kitaifa, Msonde alisema: “Tumejitahidi kwani ni asilimia kama moja na ushee ilibaki, walimu walifanya kazi nzuri na nina imani tutaifikia.”
Alisema watahiniwa 297,365 waliandikishwa kufanya mtihani huo wakiwamo wasichana 139,400 sawa na asilimia 46.88 na wavulana 157965 sawa na asilimia 53.12. Watahiniwa wa shule walikuwa 244,902 ikilinganishwa na watahiniwa 367,163 walioandikishwa kufanya mtihani huo mwaka 2013.
“Idadi ya watahiniwa wa shule walioandikishwa kufanya mtihani huo ilipungua kwa asilimia 33.3 ikilinganishwa na watahiniwa walioandikishwa mwaka 2013.”
“Mwaka 2012 kati ya watahiniwa 386,355 waliofanya mtihani wa kidato cha pili, watahiniwa 136,243 walirudia kidato cha pili na watahiniwa 250,112 waliendelea na kidato cha tatu ambao ndiyo waliosajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2014,” alisema na kuongeza:
“Kati ya watahiniwa 297,365 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne 2014, watahiniwa 288,247 sawa na asilimia 96.93 walifanya mtihani na watahiniwa 9,118 sawa na asilimia 3.07 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali.”
Alisema watahiniwa wa shule, kati ya watahiniwa 244,902 waliosajiliwa watahiniwa 244,410 sawa na asilimia 98.17 walifanya mtihani ambao wasichana walikuwa ni 110,603 sawa na asilimia 98.13 na wavulana ni 129,807 sawa na asilimia 98.19. Watahiniwa 4,492 sawa na asilimia 1.83 hawakufanya mtihani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni