Baadhi ya wanajeshi wakiangalia mabaki ya ndege ya kivita iliyoanguka katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Mwanza jana. PICHA: KWA HISANI YA JESHI LA WANANCHI WA TANZANIA. |
Rubani wa ndege ya kivita ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Meja Peter Lyamunda, amenusurika kifo baada ya ndege aliyokuwa akiitumia kuteketea katika uwanja wa Ndege wa kivita mkoani Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa JWTZ Makao Makuu Dar es Salaam, Meja Joseph Masanja, alisema ajali hiyo imetokea jana mchana wakati ndege hiyo ikiwa katika hatua za mwisho za kuruka hewani.
Alifafanua kuwa wakati ndegevita zikiwa katika mazoezi yake ya kawaida, ndege (mnyama) aliingia katika injini ya ndege hiyo na kuisababishia kuwaka moto.
“ Meja Lyamunda, alipogundua ndege yake inawaka moto alifanikiwa kujirusha nje kwa kutumia vifaa maalumu vya kujiokoa, ingawa amepatwa na majeraha hasa katika mguu wake lakini kwa sasa hali yake ni nzuri na anaendelea na matibabu,”alisema Meja Masanja.
Kutokana na ajali hiyo aliwaondoa hofu wananchi hususani wanaofanya shughuli zao jirani na viwanja hivyo kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni