Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma litawaweka kiti moto watuhumiwa 9 ambao ni viongozi wanaohusishwa na kashfa ya akaunti ya uchotaji wa fedha kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Viongozi hao watawekwa kiti moto kwa uwazi mwanzoni mwa mwezi ujao kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam. Habari zinaeleza kuwa watakaoitwa ni wale viongozi wote ambao wanaowajibika chini ya Sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya tume ya maadili zilieleza kuwa kwa sasa hati za kuitwa kwa watuhumiwa hao zinaandaliwa, lakini hata hivyo tume hiyo haikutoa majina ya watuhumiwa hao.
Hata hivyo sheria ya maadili ya viongozi wa umma inawabana viongozi na watumishi wa ngazi ya juu wa umma wakiwemo wabunge, majaji, wakuu wa wilaya, mikoa, majaji na mawaziri, mwanasheria mkuu.
Licha ya majina ya watuhumiwa hao kutopatikana, lakini chini ya sheria hiyo viongozi wanaowajibika kwa tume hiyo wako 27 na miongoni mwao wamo wabunge, wakuu wa wilaya, majaji na hakimu na katibu mkuu wa wizara.
Kwa hali hiyo wabunge ambao wanatarajia kusimama mbele ya tume hiyo ni wale ambao walipokea fedha kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering James Rugemarila ili waeleze mazingira ya kupewa fedha hizo.
Wabunge hao ni Mbunge wa Bariadi Magharibi Andrew Chenge aliyepokea Sh bilioni 1.6, Mbunge wa Sengerema William Ngeleja ( Sh milioni 40), Mbunge wa Muleba Kusini Profesa Anna Tibaijuka ambaye alipokea Sh bilioni 1.6 na akajitetea kuwa fedha hizo zilikuwa ni za mchango wa kulipa mkopo wa shule anayoisimamia.
Pia Profesa Sospeter Muhongo ambaye amejiuzulu uwaziri wa nishati na madini hivi karibuni; lakini anabakia na ubunge wake pia anaweza kuitwa mbele ya tume hiyo aeleze mazingira ya kuruhusu fedha zilizokuwemo kwenye akaunti ya Tegeta Escrow zichotwe kirahisi.
Wengine ni majaji Frederick Werema ambaye alikuwa mwanasheria mkuu wa Serikali naye ataeleza sababu za kuamuru fedha hizo za Escrow zichotwe. anabanwwa na kipengele kinachoeleza kuwa anatakiwa kutoa maamuzi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Jaji Werema katika sakata hilo anatuhumiwa kuvunja sheria za nchi kwa kuruhusu fedha hizo zichotwe bila kutozwa kodi jambo ambalo Mamlaka ya Mapato imedai kulikuwa na kodi ya Serikali.
Majaji wengine ni Dk John Ruhangisa na Aloycsius Mujulizi. Dk Ruhangisa na Mujulizi wao wamekiri kupokea fedha kutoka kwa Rugemarila. Dk Ruhangisa alipokea Sh Sh404.25 milioni na Jaji Aloysius K Mujulizi (Sh40.4 milioni).
Pia yumoa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko (Sh40.4 milioni) ambaye anabanwa na sheria hiyo pia anaweza kuitwa na tume hiyo.
Wabunge na majajji ambao wamekiri kupokea fedha hizo wanabanwa na kipengele kinachoeleza zawadi na fadhila kw aviongozi wa umma kuwa wanatakiwa wasiombe wala kupokea fadhila za kiuchumi zaidi ya zawadi ndogo ndogo ukarimu wa kawaida au fadhila nyingine za zawadi za kawaida.
Pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi naye anaweza kuitwa kwenye tume hiyo kwa kuwa bado ni mtumishi wa serikali ambaye anaendelea kuchunguzwa. Naye anabanwa na kipengele cha utoaji wa maamuzi aliyoyafanya akiwa madarakani.
Kamishna wa Tume ya Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda licha ya kukiri kuwepo kwa suala hilo lakini hakutaka kutoa ufafanuzi wa kina, lakini taarifa kutoka ndani ya ofisi ya tume ya maadili zinasisitiza kuwa kikao hicho kitafanyika mwanzoni mwa mwezi ujao .
Katika kikao hicho pia viongozi wengine wawili ambao ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mrisho Gambo ambaye ataendelea kubanwa na tume hiyo kwa madai ya matumizi mabaya ya madaraka pamoja na Meya wa Manispaa ya Tabora Gullam Hussein Dewji ataendelea kubanwa juu ya ufujaji wa fedha za manispaa anaodaiwa kuufanya
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni