promotion

Jumatatu, 22 Desemba 2014

Warioba: Nyerere angefufuka leo angeniunga mkono

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema mapendekezo ya Rasimu ya Katiba mpya yaliyofanywa na tume yake, yangeungwa mkono hata na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Warioba alisema Katiba Pendekezwa ina mambo mengi mazuri lakini pia mengi mabaya kutokana na kutengenezwa kinafiki, kiuoga na kutetea maslahi binafsi.

Akizungumza katika mdahalo uliohusu mambo yaliyomo katika Katiba Pendekezwa, Jaji Warioba alisema, mapendekezo ya tume aliyoongoza ni mazuri ambayo yangeungwa mkono na Mwalimu Nyerere hata kama ‘atafufuka’ leo.

“Wanaonipinga wanasema ninatafuta nafasi, lakini hawajibu hoja zaidi ya kusema namsaliti Mwalimu Nyerere…huyo Mwalimu akifufuka leo lazima ataniunga mkono,” alisema Jaji Warioba huku akishangiliwa.

Alisema Mwalimu Nyerere katika Azimio la Arusha alitamka kiongozi anayeishi nyumba ya kupanga hatakiwi kuwa kiongozi huku akifahamu yeye amejenga ya kwake.

“Mwaka 1984 wakati akitangaza kung’atuka urais wa nchi, akasema kuwapo na ukomo wa urais huku akifahamu muda wake wa kuitumikia nchi unamalizika mwaka unaofuata…sasa kwa mapendekezo ya tume lazima angetuunga mkono,” alisema.

Aidha, alisema katika Katiba Pendekezwa yameongezwa mambo mengi ambayo hayana msingi kwa taifa.

Alisema katika Katiba Pendekezwa, sehemu ya tunu ya taifa pamoja na Mtanzania kutotaka matabaka na kuweka uzalendo mbele, lakini wameweka kama moja ya misingi ya utawala bora.

“Tunu ya taifa haiwezi kuwa sehemu ya misingi ya utawala bora, hayo yamewekwa na wananchi yatawasilishwa kwenu,” alisema.

Alisema yapo mambo ambayo yatasababisha ‘uonevu’ kama kiongozi wa nchi atapopewa zawadi na kufanya mambo mali yake badala ya taifa.

Alisema Tume yake ilipendekeza mwiko kwa kiongozi kupokea zawadi na kufanya yake  badala ya kuwa mali ya taifa, mambo hayo yataendelea kuwapo kama wanavyoweka pesa katika akaunti za nje badala ya mabenki ya hapa nchini.

BUTIKU
Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiki, alisema Katiba haiwezi kutengenezwa kwa maslahi ya watoto wako, huo ni unafiki na uwoga na kwamba ni lazima itengenezwe kwa maslahi ya Taifa na wananchi wote.

Alisema mambo yaliyomo katika Katiba Pendekezwa yanatakiwa kujadiliwa na kuangaliwa kwa mapana ili kila mwananchi aweze kuisoma na kisha kuipigia kura itakapoingia mtaani.

ALI SALEH
Aliyekuwa mjumbe tume hiyo, Ali Salehe, akielezea nafasi ya Zanzibar katika Katiba Pendekezwa, alisema Muungano usiwe wa kulazimishwa kwani waliingia kwa hiyari na wala si kulazimishwa na kuonekana mateka.

“Ndiyo maana hata jaji mkuu wa Zanzibar alipojiuzulu, Bara hawakushituka zaidi ya huko visiwani, ndivyo ilivyokuwa kwa jaji Fredrick Werema alivyojiuzulu Bara wananchi wa visiwani hawajashituka kabisa,” alisema Saleh.

Alisema mawaziri wanaoitwa wa Muungano toka Bara, hawana nafasi yoyote kwa Zanzibar na hivyo mapendekezo yaliyofanywa na Tume ya mabadiliko ya Warioba yalikuwa sahihi kuwatenganisha vyeo hivyo kwa uwapo wa serikali tatu.

“Ndiyo maana suala la akaunti ya Escrow, wabunge 75 wa Zanzibar hawakuchangia lolote zaidi ya mmoja, kwa mtazamo wa nje linaonekana ni la Muungano, lakini hakuna kitu,” alisema.

Wengine waliochangia katika mdahalo huo ni  Humphrey Polepole, Prof. Paramagamba Kabudi na Prof. Mwesiga Baregu

.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Hakuna maoni: